Home » » MANSOUR HIMID APEWA DHAMANA ZANZIBAR

MANSOUR HIMID APEWA DHAMANA ZANZIBAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

MAHAKAMA ya Mkoa Vuga, imemwachia kwa dhamana aliyekuwa Waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Mansour Yussuf Himid ambaye anakabiliwa na makosa matatu likiwemo la kukutwa na silaha, risasi za bastola na gobore (marisau).

Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Abraham Mwampashi, jana asubuhi aliagiza mshtakiwahuyo kupewa dhamana ambapo Hakimu wa Mahakama ya Vuga, Khamis Ramadhan Shaaban,alimtaka Bw. Himid kutekeleza masharti ya dhamana.

Masharti hayo ni kuweka bondi ya sh. milioni tatu taslimu na wadhamini wake wawili kila mmoja asaini sh. milioni tano, mshtakiwa kukabidhi mahakamani hati zake za kusafiria na kuiarifu mahakama wakati anapotaka kusafiri.

Awali, mshtakiwa huyo, alinyimwa dhamana kwa sababu kosa lake la kwanza kwa mujibu wa sheria kutoruhusu apewe dhamana hata hivyo, mawakili wake Gaspa Nyika na Omar Saidi, walipeleka ombi maalumu Mahakama Kuu kuomba mteja wao apewe dhamana jambo ambalo lilikubaliwa.

Kabla ya kufikishwa mahakamani hapo jana, mshtakiwa alifikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar ambapo Jaji Mwampashi, alisikiliza ombi lake la dhamana ambalo liliwasilishwa wiki iliyopita.

Akitoa uamuzi wa ombi hilo, Jaji Mwampashi alisema Mahakama imekubaliana na ombi lake kwa mujibu wa kifungu cha 150 (4) cha sheria namba 7 ya mwaka 2004 ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Wiki iliyopita, mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka matatu na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Bw. Maulid Ali.

Bw. Ali alisema Agosti 2 mwaka huu, saa saba mchana maeneo ya Chukwani, Wilaya ya Magharibi, mshtakiwa alikutwa na silaha aina ya bastola yenye namba F76172 W, kinyume na kifungu cha 6(3) na 34 (1) (2) cha sheria ya silaha na risasi namba 2 ya mwaka 1991, sura ya 223 sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kosa la pili ni kupatikana na risasi za moto 295 za bastola; jambo ambalo ni kosa kisheria na kosa la tatu, kupatikana na risasi 112 za gobore aina ya shotgun badala ya risasi 50 alizotakiwa kuwa nayo kisheria lakini aliyakana makosa yote.

Chanzo;Majira

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa