Home » » KINANA: VIONGOZI CCM WAFITINI, WABAGUZ

KINANA: VIONGOZI CCM WAFITINI, WABAGUZ

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amekemea dhambi ya fitina na ubaguzi ndani ya chama hicho. Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika ziara yake wilayani Mafia, Kinana alisema fitina, ubaguzi miongoni mwa viongozi, zimekuwa chanzo cha kuwavuruga watu badala ya kuwatafutia maendeleo.
“Acheni, acheni dhambi ya kuwagawa na kuwasumbua watu. Punguzeni maneno na vijineno, CCM mnaongoza kwa vijineno, mnakoroga watu” alisema.
Kauli ya Kinana imetokana na kuwapo taarifa za mgogoro baina ya viongozi katika wilaya hiyo, hali inayorudisha maendeleo ya wananchi. Alisema kuwa fitina hizo, zinatokana na baadhi ya viongozi kutaka kutafuta madaraka na kupanga safu ya uongozi.
“Kazi yetu kutafuta uongozi, kupanga madiwani, mnakoroga watu, watu wanataka maendeleo, kuachana na umasikini, ninyi mnahangaika na vyeo, acheni kubeba watu. Kinana aliwaambia wananchi:
“Ukiona kuna mtu anakuja nyumbani kwako akiwa amembemba mtu, mwambie acha hayo, mimi nataka barabara ijengwe, akija mtu na maneno, mwambie hospitali hazina dawa, nataka dawa acha maneno.”
Alisema taarifa alizonazo ni kuwa kumekuwapo na migogoro ya viongozi wa CCM.
“Hamuwezi mkaendelea wakati viongozi wanakoroga watu vichwa. Leo hadithi hii kesho hadithi hii, watu wanataka kujua umeme unakuja lini, meli inakuja lini, lakini ninyi ni vyeo, vyeo, vyeo tumewapa mnatusumbua.
“CCM mna madhambi, mnakoroga watu, wanachama na viongozi wenzangu wa Chama cha Mapinduzi ndio wakorogaji wakubwa, halafu mtasingizia CUF, mtasingizi CHADEMA wakati mikorogo inaanzia kwenu,” alisema.
Kinana alisema ofisini kwake Lumumba, Dar es Salaam, kumejaa lundo la barua kutoka Mafia, zilizojaa malalamiko na fitina.
“Ofisini kwangu Lumumba nina kilo 20 za barua kutoka Mafia, kila mtu analalamika, huyu ana mlalamikia huyu, huyu anamfitini huyo” alisema.
Aidha, Kinana aliwataka wana-CCM kubadilika na kujua kuwa wananchi wanataka maendeleo na kujiondoa katika umasikini.
“WanaCCM badilikeni, hawa wananchi wanataka maendeleo, wanataka kuondokana na umasikini. Wanaongoza nchi ni sisi, wanaoulizwa maswali ni sisi, lakini badala ya kushughulika na maendeleo yao, tumeishia kuvutana mguu huyu akisongea mbele huyu anamvuta mguu.
“Badala ya simu kutumia kwa mawasiliano yenye tija, mtu anaomba aweke kwenye simu shilingi elfu arobaini kwa ajili ya kuzungumzia habari za fitina na kupigiana chapuo nani anafaa kuwa diwani, muda huo bado. Vijana hawana shida ya udiwani, shida yao ni kutafuta riziki,” alisema.
Alikemea tabia ya kuwakwamisha wale watu wanaochangia maendeleo katika wilaya hiyo, kwa hisia kuwa huenda wanataka uongozi katika kazi yoyote.
“Watu wanaoleta maendeleo, mnawapiga vita, watu wanajenga shule mnasema usijenge, akitaka kujenga kisima cha maji anaambiwa acha, fitina tu. Mafia yenye watu 46,000 mtapiga hatua sana mkishikamana”, alisema.
Kinana alitaka viongozi na wana-CCM kushikamana na kuwa na umoja ili kuleta utulivu na kuelekeza nguvu katika maendeleo.
“CCM mkitulia, Mafia itatulia, mnabaki CCM Nambari Wani, haiwi, itakuwa Nambari 10 kama mtaendekeza fitina zenu, kisiwa cha wananchi elfu arobaini kitapiga hatua kama mtashikamana na kuwa na umoja,” alisema.
Aliwataka wananchi kuwapinga vikali viongozi wanaoendekeza fitina na ubaguzi kwa kukataa hoja zao za kuvuruga watu.
“Akija kukwambia siasa, mwambie toka nje. Kuna akina mama wanafanyabiashara wanasumbuliwa na kodi, shule zina matatizo, hayazungumzwi, unazungumzia madaraka, mashamba yanachukuliwa, nanyi mko hapahapa. Acheni, acheni, mnasumbua watu, CCM inatakiwa kuwa na umoja na kushikamana” alisema Katibu Mkuu.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa