Home » » Maalim Seif: Jeshi la Polisi halitendi haki.

Maalim Seif: Jeshi la Polisi halitendi haki.


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa madai ya kwamba halitendi haki kwa vyama vya siasa.
 
Lawama hizo alizitoa juzi wakati akiwahutubia wananchi, baada ya kufungua ofisi mpya ya Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Dole, Wilaya ya Magharibi, Unguja.
 
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema mwanzoni baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa 
Zanzibar, Jeshi  la Polisi lilikuwa likifanya kazi zake bila ya upendeleo, lakini kwa sasa limetekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
 
Alisema anasikitishwa kuona Jeshi la Polisi limeingia katika siasa kwa kuviwekea vikwazo vyama vya siasa kutofanya mikutano na kuzuia watu kutoka wilaya moja kwenda nyingine kuhudhuria mikutano ya vyama hivyo.
 
Alisema Jeshi la Polisi halipaswi kuwazuia kufanya mikutano ya hadhara kwani ni haki yao kikatiba na kisheria kwa mujibu wa sheria namba tano ya vyama vya siasa nchini ambayo inasema vyama vina haki ya kufanya mikutano pahali popote.
 
“Tunaliambia Jeshi la Polisi lisiturejeshe tulipotoka, kwani kuna watu hawataki maridhiano katika nchi yetu hii na polisi mmekuwa mkiwafuata watu hao wasiotaka maridhiano,” alisema.
 
Alisema CUF kitaendelea kufanya mikutano yake ya kuwahamasisha wananchi mpaka mamlaka kamili ya Zanzibar  yatakapopatikana na hilo haliwezi kuzuilika.
 
Alisema Zanzibar haina utawala bora, lakini Oktoba mwaka huu utawala bora utapatikana na kwamba CUF itaongoza dola chini ya mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa.
 
Akizungumzia kuhusu viongozi wanaowataka katika chama hicho, alisema hawataki kuona viongozi mizigo ambao wanajinufaisha wao binafsi badala ya chama na wananchi.
 
Aliwataka wananchi hao anapotokea mtu katika chama hicho anataka uongozi wampime uwezo wake kama anafaa kukitumikia chama na wananchi na sio kujinufaisha yeye binafsi.
 
“Wapo baadhi ya viongozi wamehama hata katika majimbo yao na wanajinufaisha wenyewe badala ya kukinufaisha chama na wananchi, viongozi hawa hatuwataki katika uchaguzi mkuu,” alisema Maalim Seif. 
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa