Na Is-haka Omar, Zanzibar.
WAJUMBE
wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kaskazini Unguja Kichama wametakiwa
kutumia vikao halali kama inavyoelekezwa na Katiba na Kanuni za Chama
kwa kuwahoji na kuwachukulia hatua mwafaka baadhi ya viongozi na
wanachama wanaokwenda kinyume na misingi ya Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai na Kamati ya siasa ya
Mkoa huo katika kikao cha kuongeza ufanisi wa kiutenda huko Mahonda
Unguja, alisema viongozi hao wanatakiwa kuwa na uthubutu wa kufichua
wale wote wanaokwenda kinyume na matakwa ya Chama.
Vuai
aliwakumbusha viongozi hao kuwa wana mamlaka ya kuwachukulia hatua za
kuwaita , kuwahoji na kuwapa fursa ya kujitetea katika vikao halali vya
chama viongozi na wanachama wanaotuhumiwa kufanya vitendo vinavyokwenda
kinyume na Katiba ya CCM au maelekezo ya chama.
“Kamati
ya siasa ya Mkoa nyinyi ni ngazi ya juu kabisa ndani ya Mkoa kichama,
hivyo mnawajibu wa kuchukua maamuzi ya kuwaita baadhi ya watu
mnaowashuku kukisaliti chama katika vikao stahiki na kuwahoji na kuwapa
nafasi ya kujitetea kabla ya kuwaadhibu.”, alisema Vuai.
Vuai
alisisitiza kuwa hatua za kuwashughulikia Wanachama wa Chama hicho
wanaotuhumiwa kwenda kinyume na maadili ya Chama ni lazima kuhakikisha
hakuna Mwanaccm anayechukuliwa hatua kwa kuonewa au kudhalilishwa.
Alikemea
tabia za baadhi ya Wana CCM kuitana wasaliti bila ya kuwa na ushahidi
wa kutosha katika kuthibitisha tuhuma hizo, kwani zinaweza kukwamisha
utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na maendeleo ya Chama kwa ujumla.
“
Viongozi lazima muwe makini tunapoletewa kesi fanyeni utafti kwanza
kwani kuna tuhuma zingine zinatokana na chuki binafsi hivyo watu
wanaona njia ya kumaliza visasi vyao ni kuwatuhumu wenzao kuwa ni
wasaliti, wakati mwingine tuhuma hizo zinakuwa hazina ukweli.”,
alisisitiza Vuai na kuongeza kuwa CCM ni chama kinachosimama katika
misingi ya ukweli na hakiwezi kufanya uonevu kwa watu wasiokuwa na
hatia.
Naibu
Katibu Mkuu huyo aliitaka Kamati hiyo kuendelea kujenga mazingira
rafiki ya kuwa karibu na viongozi wao wa ngazi za chini pamoja na
wanachama wote kwa lengo la kujua kwa undani changamoto zinazowakabili
katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alieleza
kwamba misingi ya Demokrasia, nidhamu na uwazi uliojengeka ndani na
nje ya chama hicho vinatakiwa kulindwa na kuenziwa na kila kiongozi
anayekabidhiwa dhamana za kiutendaji au uongozi.
Alieleza
kuwa kazi iliyopo mbele ya chama ni kujiandaa kwa mambo mbali mbali
yakiwemo Uchaguzi wa ndani wa CCM wa mwaka 2017, kwa ajili ya kupata
viongozi makini watakaobeba jukumu la kusimamia maandalizi ya Uchaguzi
Mkuu ujao na kuhakikisha Chama hicho kinapata ushindi wa kihistoria.
Alisema
wanachama wanaokusudia kuwania nafasi mbali mbali za uongozi wa Chama
na Jumuiya zake , lazima wawe Wanaccm safi ambao hawana rekodi mbaya ya
utumishi wao ndani ya chama au serikalini hata katika nafasi zozote ya
uongozi walizowahi kutumikia hapo nyuma.
Pamoja
na hayo aliwashauri viongozi kuwa mabalozi wazuri kwa kuwasihi
wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na
serikali pamoja na kulinda amani na utulivu wa nchi.
Hata
hivyo aliipongeza Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kaskazini Unguja, kwa
juhudi zao katika kuimarisha Chama pamoja na kusimamia kwa vitendo
utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
0 comments:
Post a Comment