Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Jengo jipya la Skuli ya Sekondari ya Chambani akiwamwishoni mwa ziara yake ya siku tatu kukagua miradi ya kiuchumi na maendeleo Kisiwani Pemba. Kushoto yake ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Zahara Hamad.
Makamu wa Pili wa Rais wa Z anzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwapongeza Wakulima wa Bonde la Maziwapacha ambao hawapo pichani katika Kijiji cha Chambani Wilaya ya Mkoani. Kushoto yake ni Afisa Mdhamini wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Pemba Dr. Suleiman Sheikh pamoja na Baadhi ya Wataalamu wa Wizara hiyo.
Mshauri wa Ujenzi wa Mradi wa Matengenezo ya Skuli ya Sekondari ya Fidel Castro Pemba kutoka Kampuni ya M.S. Rans Co. LTD Bwana Nassor Al-Miskri akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika kutembelea Mradi huo. Kushoto ya Balozi Seif Ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi
----
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema mfumo unaotumiwa na Wananchi wa Jimbo la Chambani Mkoani Pemba wa kujumuika pamoja katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo bila ya kuingiza Siasa unafaa kupongezwa na wapenda Maendeleo Nchini.
Balozi Seif ameeleza kufurahishwa na mfumo huo mara baada ya kulizindua Jengo Jipya la Skuli ya Sekondari ya Chambani akiwa mwishoni mwa ziara yake ya siku tatu kutembelea miradi ya kiuchumi na Maendeleo Kisiwani Pemba.
Alisema mfumo huo unasaidia kuachana na Siasa kwenye masuala ya Maendeleo hasa lile la Elimu ambalo ndio Dira kwa ufanisi wa Wanafunzi wao hapo baadaye.
“ Achaneni na Siasa katika masuala ya Maendeleo hasa lile la Elimu”. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliipongeza Kamati ya Skuli ya Chambani kwa jitihada zake za kuwajengea mazingira mazuri ya Kielimu Watoto wao na kuwataka kuongeza nguvu kwenye ujenzi wa Nyumba za Walimu ili kuwarahisisha Wanafunzi hao kuwa karibu na Walimu wao kwa muda wote.
Balozi Seif aliwaasa Wazazi kuachana na tabia ya kuwaozesha waume watoto wao mapema kwani kufanya hivyo ni kuwavurugia hatma yao ya kimaisha hapo baadaye.
“ Tumekuwa tukiishuhudia tabia hii ndani ya Jamii inayofanywa na baadhi ya Wazazi kuwaozesha Watoto wao wakiwa wanaendelea na Masomo na wengine wamebahatika kuwa na kipaji kinachowawezesha kufikia ngazi ya chuo Kikuu”.Alifafanua Balozi Seif.
Katika Risala yao Wananchi hao wa Jimbo la Chambani wameiomba Serikali Kuu kufikiria njia za kusaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo Jimboni humo likiwemo lile la ubovu wa Bara bara.
Wananchi hao walimueleza Balozi Seif kwamba ukosefu wa Bara bara ya uhakika Kijijini humo unapelekea kuviza kwa harakati zao za kila siku za maendeleo.
Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ,Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali Mh. Zahara Hamad aliahidi kwamba Wizara hiyo itajitahidi kuona Jengo lililomalizika kujengwa kwa nguvu za Wananchi wa Jimbo hilo linakamilishwa kuezekwa na Wizara kama utaratibu ulivyowekwa.
Mh. Zahra aliwaeleza Walimu na Wanafunzi wa Skuli hiyo kwamba Wizara ya Elimu imo katika jitihada za kushirikiana na wahisani kwa lengo la kufanikisha Mradi wa Tanzania ishirini na moja { Tanzania Twenty First } unaokusudiwa kuewawezesha Wanafunzi kujifunza Kompyuta na Walimu kufundisha kwa Kompyuta.
Katika hafla hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alihamasika na kuahidi kuchangia shilingi Milioni 2,000,000/- kwa ajili ya uendelezaji wa Jengo jengine Jipya la Skuli hiyo na Shilingi 500,000/- kusaidia Kituo cha Maandalizi cha Skuli ya Chambani.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikagua Ukulima wa Mpunga wa kutegemea Mvua katika Bonde la Maziwa pacha Chambani na kuwapongeza Wakulima wa Bonde hilo kwa hatua zao za kuimarisha Kilimo cha Mpunga.
Akisalimiana na Wakulima wa Bonde hilo Balozi Seif alisema Serikali iko mbioni katika kuelekeza nguvu zake kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa kukamilisha miundo mbinu itakayofanikisha mpango huo.
Alisema kilimo cha umwagiliaji kinamuwezesha Mkulima kuendeleza Kilimo hicho katika misimu miwili kwa mwaka na kuwaongezea mapato mara mbili pamoja na chakula cha uhakika.
Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif alikagua Maendeleo ya matengenezo makubwa ya Skuli ya Sekondari ya Fidel Castrol unaofanywa na Kampuni ya Ujenzi ya Kizalendo ya M.S. Rans Co. LTD.
Mshauri wa Ujenzi wa Kampuni hiyo Bwana Nassor Al-Miskri alimueleza Balozi Seif kwamba ujenzi huo utachelewa kukamilika kama ilivyopangwa kufuatia mapendekezo mengine ya kuongezeka kwa baadhi ya Majengo katika Skuli hiyo.
Matengenezo ya Ujenzi wa Skuli ya Sekondari Fidel Castrol yanatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi Bilioni tatu.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment