Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Zanzibar ndiyo mkoa wa kwanza wenye idadi ndogo ya watu
wanaopata huduma za kifedha, licha ya kuwa na mitandao ya simu kama ile
iliyopo bara.
Ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa na Mfuko wa
Kuendeleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) inaonyesha kuwa Zanzibar
inashika mkia licha ya Tanzania kuongoza duniani kwa kutumia simu
kujipatia huduma za kifedha.
Idadi ya wanaotumia benki imeongezeka kutoka asilimia 9.1 mwaka 2009 mpaka asilimia 13.9 mwaka 2013.
Aidha, asilimia 73.2 ya watu hao wamekuwa wakipata
huduma za kifedha zinazojumuisha bima, vyama vya kuweka na kukopa na
kutuma na kupokea fedha kupitia taasisi nyingine mbalimbali
zilizoanzisha huduma za kutoa huduma za fedha.
Ongezeko hili la wanaopata huduma hizi linaonekana
zaidi kwa watu wa bara pekee kwani, kwa Zanzibar, takriban asilimia 50
hawapati huduma hizi.
Huko, asilimia 11.5 ya watu wamekuwa wakitumia
benki wakati asilimia 25.5 wamekuwa wakipata huduma hizo kupitia simu na
asilimia 17.1 wanatumia huduma nyinginezo za fedha.
Hali ni tofauti na Mkoa wa Kilimanjaro unaoongoza
kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wapatao huduma za kifedha ikifuatiwa na
Dar es Salaam.
Mkoa wa Kilimanjaro una asilimia 93.8 ya watu
wanaopata huduma za fedha ukilinganisha na asilimia 54.1 kwa Zanzibar.
Asilimia 16.8, zaidi ya wastani wa Taifa, wanapata huduma za benki huko
Kilimanjaro.
Mojawapo ya sababu za hali kuwa mbaya kwa Zanzibar ni taarifa kwamba wengi hawajishughulishi na uzalishaji.
Hii inaweza ikawa sababu ya wao kutopata huduma hizi kutokana na ukweli kwamba hawana uwezo wa kumudu gharama hizo.
Wakati Tanzania sasa ikiwa na matawi ya benki
yanayofikia 50 kote nchini na watumiaji wa simu wapatao milioni 28, kuna
haja ya watu wa visiwani kubadilika na kuondokana na mfumo huo wa
maisha.
Mitandao ya simu iliyopo, bara ipo Zanzibar pia, jambo linalotoa fursa sawa kwa wote.
Licha ya kwamba ripoti hiyo inaonyesha watu wengi wanahifadhi
fedha zao nyumbani, bado wanatuma na kupokea fedha kwa kutumia njia
tofauti na hata kufanya malipo pia kwa njia hizo, mfano m-pesa, airtel
money, tigo pesa na hata easy pesa.
Pamoja na sababu nyingi za Watanzania wengi
kutotumia huduma hizi, bado kuna kila haja ya kubadilika na kutoishi
kijima kwani uchumi wa nchi hii unakua na mwingiliano na mataifa mengine
unaongezeka.
Kutokuwa na fedha za kutosha, umbali wa kufuata
huduma na gharama kubwa za huduma hizo kumekuwa kukielezewa kuwa ni
kikwazo kwa watu wengi kumudu huduma hizo wakati wa zoezi la ukusanyaji
wa taarifa za utafiti huo.
Wakati taasisi za fedha zikishauriwa kuangalia
gharama za huduma zao, wananchi hawana budi kubadilika ili kuendana na
mfumo mpya wa dunia unaohamia ulimwengu wa malipo kwa njia ya mtandao
(cashless economy). Kampuni ya simu nazo, kwa kuwa ni rahisi kutumia
simu, ni vyema zikaiona fursa hii na kuitumia.
Elimu ya huduma hizo ni tatizo kubwa kwa wananchi
wengi hasa tukizingatia kuwa theluthi moja ya Watanzania wote hawajui
kusoma wala kuandika kama ilivyobainishwa hivi karibuni na Shirika la
Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).
Kimsingi kuna kila sababu kwa Tanzania kuangalia
namna gani inaweza kufanya ili kuharakisha maendeleo nchini hasa katika
sekta hii ya fedha.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment