Mwenyekiti wa Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis amesema baadhi ya
viongozi ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wameshindwa kutekeleza wajibu
wao.
Amesema wajibu huo
ni pamoja na kushindwa kutatua kero za madaktari na kusababisha kuzorota
kwa huduma za afya visiwani humo. Sadifa aliyasema hayo jana alipokuwa
akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Vuga katika Mkoa wa Mjini
Magharibi, Unguja.
“Serikali imekuwa
ikitumia gharama kubwa kumhudumia kwa matibabu, Makamu wa Kwanza wa Rais,
Maalim Seif Sharrif Hamad, itakumbukwa aliwahi kuwaahidi wananchi wa Zanzibar
kuwa akiwa kiongozi atahakikisha anatibiwa hapa hapa badala ya kusafirishwa nje
ya nchi,” alisema.
Wabara waishio Zanzibar
Kiongozi huyo wa UVCCM,
alisema watu wa Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar, si wakimbizi kwa mujibu wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Sadifa alisema wapinzani
wanaohoji uhalali wa watu hao kuishi na kufanya kazi Zanzibar, hawafahamu haki
ya kila mtu kikatiba kwa maana ya kuwa huru kuishi na kufanya kazi katika
sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema ibara ya 11 na 26 ya
katiba imeweka wazi kwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi sehemu atakayo ndani
ya Jamhuri ya Muungano.
Huku akishangiliwa na
wanachama wa CCM alisema sera za ubaguzi hazitasaidia kujenga amani na umoja wa
kitaifa baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Novemba mwaka 2010.
Naibu Katibu Mkuu wa
UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, alisema umoja huo umeamua kuchunguza kikundi
cha watu wenye asili ya India ambao wamekuwa wakipinga misingi ya Mapinduzi
na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema ni jambo la
kushangaza kuona watu hao wakiwa katika mstari wa mbele kuhoji uhalali wa
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wakati hakuna muafrika anayeweza kwenda
kuhoji uhalali wa harakati za ukombozi wa India au Iran kama hali
ilivyojitokeza visiwani Zanzibar.
Alisema kitendo hicho
hakikubaliki
CHANZO MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment