Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif
Sharif Hamad, amelitupia lawama Jeshi la Polisi kwa madai ya
kwamba halitendi haki kwa vyama vya siasa.
Lawama hizo alizitoa juzi wakati akiwahutubia wananchi, baada ya
kufungua ofisi mpya ya Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Dole, Wilaya ya
Magharibi, Unguja.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema mwanzoni baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Zanzibar, Jeshi la Polisi lilikuwa likifanya kazi zake bila ya
upendeleo, lakini kwa sasa limetekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema anasikitishwa kuona Jeshi la Polisi limeingia katika siasa
kwa kuviwekea vikwazo vyama vya siasa kutofanya mikutano na kuzuia watu
kutoka wilaya moja kwenda nyingine kuhudhuria mikutano ya vyama hivyo.
Alisema Jeshi la Polisi halipaswi kuwazuia kufanya mikutano ya
hadhara kwani ni haki yao kikatiba na kisheria kwa mujibu wa sheria
namba tano ya vyama vya siasa nchini ambayo inasema vyama vina haki ya
kufanya mikutano pahali popote.
“Tunaliambia Jeshi la Polisi lisiturejeshe tulipotoka, kwani kuna
watu hawataki maridhiano katika nchi yetu hii na polisi
mmekuwa mkiwafuata watu hao wasiotaka maridhiano,” alisema.
Alisema CUF kitaendelea kufanya mikutano yake ya kuwahamasisha
wananchi mpaka mamlaka kamili ya Zanzibar yatakapopatikana na hilo
haliwezi kuzuilika.
Alisema Zanzibar haina utawala bora, lakini Oktoba mwaka huu
utawala bora utapatikana na kwamba CUF itaongoza dola chini ya mfumo wa
serikali ya umoja wa kitaifa.
Akizungumzia kuhusu viongozi wanaowataka katika chama hicho,
alisema hawataki kuona viongozi mizigo ambao wanajinufaisha wao binafsi
badala ya chama na wananchi.
Aliwataka wananchi hao anapotokea mtu katika chama hicho anataka
uongozi wampime uwezo wake kama anafaa kukitumikia chama na wananchi na
sio kujinufaisha yeye binafsi.
“Wapo baadhi ya viongozi wamehama hata katika majimbo yao na
wanajinufaisha wenyewe badala ya kukinufaisha chama na wananchi,
viongozi hawa hatuwataki katika uchaguzi mkuu,” alisema Maalim Seif.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment