Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wakuu wa Jeshi la Polisi wa Nchi za SADC Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Wakuu wa Jeshi la Polisi wa Nchi za SADC ambao wapo Zanzibar kwa Kikao chao cha Nne cha Jumuiya hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya Pamoja na Wakuu wa Jeshi la Polisi la Nchi wanachama wa SADC mara baada ya mazungumzo yao. Kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Said Mwema na Wa pili kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed akifuatiwa na Mwenyekiti wa Mkutano huo Mkuu wa Jeshi la Polisi la Rwanda Bibi Mangurashi Riah Phyiyega.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Ujumbe wa Kamati Tendaji ya Mabaraza ya Habari Duniani { WAPC } Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Ujumbe huo ulikuwepo Zanzibar kwa ziara ya siku mbili kutembelea sehemu ya Kihistoria.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Kamati Tendaji ya Mabaraza ya Habari Duniani { WAPC } uliofika ofisini kwake kwa mazungumzo.(Mpiga Picha- Saleh Masoud Mahmoud – OMPR- ZNZ).
Na. Othman Khmais Ame
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema nguvu za ziada zinahitajika kuchukuliwa kwa pamoja katika kukabiliana na wimbi la Dawa za kulevya ambalo linaonekana kuiathiri nguvu kazi kubwa ya Bara la Afrika ambayo ni Vijana.
Balozi Seif ameeleza hayo katika mazungumzo yake na Wakuu wa Jeshi la Polisi wa Nchi Wanachama wa Mataifa ya Jumuiya ya Nchi za Kusini, Kati na Mashariki mwa Bara la Afrika { SADC } Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Kundi kubwa la Vijana linaonekana kutumbukia katika matumizi ya Dawa za kulevya hali ambayo inatishia kudumaa kwa Uchumi wa Mataifa hayo wanachama hapo baadae.
“ Nguvu kazi kubwa ya uchumi wa Nchi yoyote ile hutegemea zaidi Vijana. Sasa hali hii ya kutowadhibiti Vijana hao katika janga hili Mataifa yetu yategemee nini?”. Alihoji Balozi Seif Ali Iddi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wakuu hao wa Polisi wa Nchi wanachama wa Sadc kuendelea kushirikiana pamoja ili kuondoa ile dhana kwamba Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika ni mlango mkuu wa kupitishia Dawa za kulevya kutoka Bara moja hadi jengine.
Alisisitiza kwamba ipo haja ya kuongezwa nguvu zaidi katika maeneo ya mipaka na Bandari kwa kutumia Taaluma ya kisasa ili kupunguza au kuondosha kabisa biashara hiyo haramu.
Akizungumzia uharamia ulioikumba Pembe ya Bara la Afrika pamoja na migogoro ya Mipaka Balozi Seif aliomba busara za kidiplomasia zikatumia zaidi katika kuona changamoto hizo zinapatia ufumbuzi. Alisema hali ya Maisha na Mali za Wananchi hasa Wafanyabiashara zimekuwa mashakani na endapo tabia hiyo kama haikudhibitiwa inaweza kusababisha kuporomoka kwa Uchumi wa Mataifa Wanachama wa Sadc.
Aliupongeza Uongozi wa Wakuu wa Polisi wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini, Kati na Mashariki mwa Afrika kwa uamuzi wao wa kufanya Kikao chao cha Nne cha Jumuiya hiyo hapa Zanzibar.
Alisema uamuzi huo kwa kiasi kikubwa umeipatia heshima Zanzibar hasa kutokana na utulivu na amani iliyojengeka kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeshwa kwa mfumo wa Umoja wa Kitaifa. Mapema Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania Inspeta Generali Said Mwema alisema Washiriki wa Kikao hicho watapata fursa ya kubadilishana mawazo kufuatia changamoto wanazopambana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao likiwemo zaidi suala la kuimarishwa kwa amani ya Nchi zao.
Inspekta General Said Mwema alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba washiriki hao watajaribu kuangalia mbinu zaidi za ushirikiano ambazo wanaweza wakasaidiana katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya pamoja na suala la mipaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi la Rwanda Kamanda Mangurashi Riah Phyiyega alielezea faraja yake kutokana na mapokezi waliyoyapata yeye na Ujumbe wake tokea walipowasili hapa Zanzibar.
Bibi Mangurashi alisema kwamba wajumbe wake wameonyesha kufurahia mazingira ya Zanzibar na Watu wake ambayo yamejenga matumaini ya kumaliza kikao chao kwa njia ya mafanikio makubwa.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana na Wajumbe wa Kamati Utendaji ya Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani { WAPC } uliopata fursa ya kufanya ziara ya siku mbili kuitembelea Zanzibar.
Katika mazungumzo na Ujumbe huo Balozi Seif alisema watendaji wa Sekta ya Habari wanapaswa kuendelea kuheshimu maadili ya fani yao kwa vile wamebeba dhima kubwa ya kuzipatia Jamii zao Taaluma. matukio pamoja na Habari zilizowazunguuka.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Sekta ya Habari ni muhimu katika Jamii, hivyo wanataaluma wa fani hiyo wana wajibu wa kuhakikisha elimu na Taarifa wanazozitoa zinakuwa sahihi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif amewapongeza wana habari wa Tanzania kwa kazi kubwa wanayotekeleza kwa jamii na Taifa kupitia mfumo wa uhuru wa Habari uliopo Nchini.
Mapema Kiongozi wa Ujumbe huo wa Kamati Utendaji ya Umoja wa Mabaraza la Habari Duniani Bwana Chris Conybeare alisema ziara ya ujumbe wake imefanikiwa vyema kutokana na wana habari hao kupata mwanga wa kuielewa Historia ya Zanzibar.
Bwana Chris alifahamisha kwamba Zanzibar imebarikiwa kuwa na utajiri wa Historia inayopaswa kutumiwa na Jamii ya Kimataifa popote pale.
Kwa pande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania { MCT } Bwana Kajubi Mukajanga ambaye ni mwenyeji wa Ujumbe huo alisema Tanzania imepata bahati ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kamati hiyo mwaka huu.
Katibu Mtendaji Kajubi alifahamisha kwamba Kamati tendaji ya Umoja huo wa Mabaraza la Habari Duniani { WAPC } imeshawahi kufanya Mikutano yake katika Mataifa ya Nepal na Cyprus.
0 comments:
Post a Comment