Home » » Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali idd:''Ntahakikisha kwamba Sekta ya Michezo inapata nguvu zaidi kutokana na umuhimu wake uliojichomoza hivi karibuni wa kutoa ajira ..''

Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali idd:''Ntahakikisha kwamba Sekta ya Michezo inapata nguvu zaidi kutokana na umuhimu wake uliojichomoza hivi karibuni wa kutoa ajira ..''



Mwakilishi wa Timu ya Soka ya Kitope United akipokea msaada wa Seti ya
Jezi pamoja na Fedha Taslimu kwa ajili ya usajili na kujiandaa kwenye
mashindano yanayowakabili.
  Makamu wa pili wa Rais Zanzibar na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na
wanamichezo wa Timu nne za soka za Jimbo la Kitope hapo ukumbi wa Tawi
la CCM la Kitope A.
Khamis Mswahili Mwinyi Mwakilishi wa wanamichezo wa timu nne za soka za
Jimbo la Kitope akiwasilisha changamoto wanazokabiliana nazo katika
michezo kwa Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi. 
--

Uongozi wa Jimbo la Kitope umekusudia kuimarisha sekta ya michezo kwa
lengo la kuwawezesha Vijana wa Jimbo hilo kuwa pamoja katika harakati
zao za Michezo na zile za kijamii. 

Makamu wa pili wa Rais Zanzibar na  Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo mara baada ya
kupokea matatizo na ushauri wa wanamichezo wa Timu Nne zilizomo ndani ya
Jimbo hilo walioutoa katika Kikao chao kilichofanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa Ofisi ya Tawi la CCM Kitope A. 


Balozi Seif aliwaeleza wawakilishi wa Timu hizo ambazo ni Kitope United,
African Boys, Home Boys na Kombora kwamba uamuzi wao wa kufikiria
kuanzisha Timu moja imara ndani ya jimbo hilo umetoa faraja kwa
viongozi jambo ambalo litarahisisha hata upatikanaji wa vifaa na misaada
kwa wepesi zaidi.


 Aliahidi kwa kuwa yeye ni Kiongozi wao wa Jimbo atahakikisha kwamba
Sekta ya Michezo inapata nguvu zaidi kutokana na umuhimu wake
uliojichomoza hivi karibuni wa kutoa ajira endapo Vijana hao watajituma
vilivyo.
“ Nataka kuona Timu za Jimbo langu la Kitope zinashiriki na kufanya
vizuri katika mashindano ya Wilaya, Mikoa na hata Taifa. Lakini
kitachosaidia zaidi kwenu ni juhudi ya kuzingatia mazoezi
yatakayofuatiwa na nguvu za misaada ya Viongozi wenu”. Alisisitiza
Balozi Seif. 


Akizungumzia matatizoyanayozikabili Timu hizo Balozi Seif atajaribu
kuzungumza na wafadhili mbali mbali wa michezo ili kuona namna gani
wanaweza kusaidia uimarishaji wa uwanja wa uhakika na wa kisasa ndani ya
jimbo hilo. 


Alisema suala hilo litakwenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya
michezo ikiwemo Mipira, Nyavu Magoli na Jezi ambazo alisema zimo ndani
ya uwezo wake kulingana na utaratibu aliokwishauanzisha tokea alipoanza
kuliongoza jimbo hilo. 


Kuhusu suala la uanzishwaji wa jengo la kudumu la Klabu Balozi Seif
aliwaagiza wanamichezo hao kuanza shughuli za maandalizi ya msingi kwa
vile tayari wameshaanza kukusanya nguvu za pamoja.
Alisema katika kuunga mkono jitihada hizo za wanamichezo atahakikisha
anasaidia nguvu za unyanyuaji jengo kwa hatua ya matofali na kuangalia
mbinu za kuendeleza ujenzi huo.


 Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwakumbusha wanamichezo hao kuwa waangalifu kutokana na ushawishi
wanaoendelea kusambaziwa wa kutaka kuingizwa katika vurugu za kisiasa
kwa kisingizio cha Kidini.
Balozi Seif alitahadharisha kwamba ushawishi huo unaweza kuyayusha
kabisa amani na muda wa Vijana hao wa kushiriki kikamilifu katika
michezo yao endapo wataamua kuupokea.


 Mapema wanamichezo hao walimueleza Balozi Seif matatizo yanayowakabili
katika katika harakati zao za kuendeleza michezo ambayo yamekuwa
yakipunguza kasi yao ya ufanisi.
Wawakilishi wa wanamichezo hao Khamis Mswahili Mwinyi, Ngamia Mohd
Ngamia na Amour Amour kwa pamoja walielezea changamoto zinazowakabili
katika sekta ya michezo ikiwa ni pamoja na uhaba wa vifaa vya michezo,
ujenzi wa Jengo la Klabu pamoja na uanzishwaji wa mashindano ya kombe la
Mbunge wa Jimbo hilo ambayo tayari yamesharidhiwa na Mbunge mwenyewe
kwa kukubali kutoa Vikombe na zawadi kwa washindi.


 Walisema kufanikiwa kwa changamoto hizo kutawawezesha Vijana waliowengi
wa jimbo hilo kuwepuka kusambaratika pamoja na vishawishi vinavyoweza
kuwapelekea kujiingiza katika matendo maovu. 


Katika kikao hicho Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi
alikabidhi seti ya Jezi na Fedha Taslimu kwa Timu ya Soka ya Kitope
United inayojiandaa na usajili kwa ajili yua mashindano yajayo. 
Na

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa