Home » » WARIOBA AZIDI KUWAONYA WANASIASA, *AWATAKA WASIWALISHE MAWAZO WANANCHI *ASISITIZA KATIBA MPYA KUPATIKANA APRILI, 2014

WARIOBA AZIDI KUWAONYA WANASIASA, *AWATAKA WASIWALISHE MAWAZO WANANCHI *ASISITIZA KATIBA MPYA KUPATIKANA APRILI, 2014

Na Mwandishi Wetu
TUME ya Mabadiliko ya Katiba imesisitiza umuhimu wa wadau mbalimbali, wakiwamo wanasiasa, kuwaacha wananchi kutoa maoni yao binafsi katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, alitoa onyo hilo tena jana, alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Baraza la Wawakilishi ZanzĂ­bar.

Jaji Warioba aliwataka wanasiasa kuacha mchezo huo na kusisitiza kuwa makundi na taasisi mbalimbali zitapata nafasi ya kukutana na tume na kutoa maoni yao.

Warioba alisema changamoto kubwa ambayo tume hiyo inakabiliana nayo ni wananchi kupewa mawazo ya kuzungumza na watu wengine, jambo ambalo haliwasaidii wananchi.

“Makundi ya watu, taasisi za kiraia na hata vyama vya siasa vimekuwa mstari wa mbele kuwalisha wananchi mambo ya kuzungumza,” alisema.

Jaji Warioba aliwataka wawakilishi hao kuisaidia tume hiyo kuwaelimisha wananchi kuwa tayari kutoa maoni yao ya moyoni na kukataa kupokea mawazo ya watu wengine ili Katiba itakayopatikana iwe inawakilisha mawazo yao.

Jaji Warioba alikuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ali Abdalla Ali, ambaye alitaka kujua changamoto ambazo tume hiyo inakutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Jaji Warioba alisisitiza kuwa viongozi wa makundi mbalimbali wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi kutoa maoni yao binafsi badala ya kuwaelekeza aina ya maoni wanayopaswa kuyatoa.

Akizungumzia kuhusu muda uliopangwa katika kutekeleza kazi hiyo, Jaji Warioba alieleza kuwa pamoja na changamoto hiyo, lakini tume yake imejipanga kumaliza kazi yake ndani ya muda uliopangwa kisheria.

“Tume imejipanga kuhakikisha ifikapo Aprili 26 2014 Katiba mpya inakuwa tayari. Kimsingi mazingira ya hali ya kisiasa nchini yanalazimisha kuwepo na Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” alisema.

Wajumbe hao wa baraza la wawakilishi wapo katika ziara ya taasisi mbalimbali za Muungano zilizopo jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ali Abdallah Ali, alisema wajumbe wa kamati watatumia uzoefu na elimu waliyoipata katika ziara yao ili kuisaidia tume hiyo kutekeleza majukumu yake.

Wajumbe hao walipata nafasi ya kutembelea kitengo cha Utafiti na Taarifa Rasmi (Hansard) cha tume hiyo, ambapo waliweza kuona jinsi maoni ya wananchi yanavyopokewa na kufanyiwa kazi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa