Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Jengo la Mahakama kuu ya Zanzibar
Mahakama Kuu ya Zanzibar imesema mashtaka ya ugaidi yanaweza
kufunguliwa katika mahakama yoyote baina ya pande mbili za Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kama ilivyotokea kwa Wazanzibari 14 waliokamatwa
Zanzibar na kufunguliwa mashtaka yao Tanzania Bara.
Akitoa uamuzi katika kesi ya maombi iliyofunguliwa
dhidi ya viongozi wa Polisi Zanzibar na washtakiwa hao 14 wanaopinga
kukamatwa Zanzibar na kufunguliwa mashtaka Tanzania Bara, Jaji wa
Mahakama Kuu ya Zanzibar, Mkusa Isaac Sepetu alisema hakuna sheria wala
Katiba iliyovunjwa.
Jaji Sepetu alisema baada ya kusikiliza hoja za
pande zote mbili, Mahakama Kuu imejiridhisha kuwa Sheria ya Ugaidi Namba
2 ya mwaka 2002, iliyotumika kuwafungulia mashtaka inatoa uwezo wa
kukamata na kufungua mashtaka katika eneo lolote la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania.
Jaji Sepetu alisema ombi la Wazanzibari hao la
kuitaka Mahakakama Kuu ya Zanzibar itoe amri kwa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kuwaachia huru watuhumiwa hao ni sawa na kuingilia uhuru wa
mahakama nyingine iliyopo katika upande mmoja wa Muungano ambayo
inatakiwa ifanye kazi bila ya kuingiliwa na upande mwingine.
Jaji Sepetu alisema ombi lililofunguliwa na
walalamikaji halina nguvu za kisheria kwa vile limefunguliwa nje ya
wakati huku watuhumiwa wakiwa wamefikishwa mahakamani siku tisa kabla
Wazanzibari hao kuwasilisha maombi yao Mahakama Kuu ya Zanzibar ya
kupinga kushtakiwa Tanzania Bara.
Jaji huyo alisema Mkurugenzi wa Mashtaka wa
Tanzania (DPP) aliwafikisha watuhumiwa mahakamani mnamo Julai 17 wakati
maombi ya Wazanzibari hao ya kupinga kukamatwa na kufunguliwa mashtaka
yao Tanzania Bara yalifunguliwa Julai 28, mwaka huu.
“Kama waombaji wanapinga uamuzi huu, wanaweza
kufungua maombi yao katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga wateja wao
kushtakiwa upande wa pili wa Muungano,” alisema Jaji Sepetu.
Vilevile, alisema Mahakama Kuu ya Zanzibar haina
mamlaka wala uwezo wa kuchukua hatua ya kuingilia uhuru wa mahakama
nyingine hasa kwa kuzingatia watuhumiwa hao hawapo tena mikononi mwa
Polisi, wapo ndani kwa amri ya Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu na
kushikiliwa katika Gereza la Segerea.
Hata hivyo, Jaji Sepetu alilitaka Jeshi la Polisi
kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na taratibu ili kuepuka
malalamiko yasiyokuwa ya lazima hususan suala la ukamataji na kuepuka
kukaa na watuhumiwa nje ya wakati kwa mujibu wa sheria bila ya
kuwafikisha mahakamani.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo, Wakili Abdallah Juma
alisema wateja wake walikamatwa na kufunguliwa mashtaka kinyume na
Kifungu cha 56 a(1)(3) kinachotoa mamlaka pekee kwa Mkurugenzi wa
Mashtaka Zanzibar kufungua na kushughulikia mashtaka yoyote ya jinai
dhidi ya mtu yeyote mbele ya mahakama yoyote isipokuwa ya kijeshi.
Alisema kitendo cha kuwakamata na kutowafikisha
katika Mahakama za Zanzibar ndani ya saa 24, kilivunja Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984, Kifungu cha 14(1) na 16(1) vinavyotoa uhuru wa
kila mtu kuwa na haki ya hifadhi ya maisha yake na kutonyimwa uhuru wake
wa kwenda popote, haki ya kuishi katika sehemu yoyote ya Zanzibar.
Wazanzibari hao 14 walifunguliwa mashtaka ya kula
njama za ugaidi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kinyume na Kifungu cha 21 cha Sheria ya Ugaidi cha Sheria Namba
2 ya mwaka 2002
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment