Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Polisi
Zanzibar inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuwatukana na
kuwakashifu viongozi wakuu wa serikali, akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk.
Ali Mohammed Shein na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makao makuu ya Jeshi la Polisi
visiwani hapa, Naibu Mkurugenzi wa makosa ya jinai (DCI), Salum Msangi,
alisema watu hao wapo chini ya ulinzi mpaka hapo upelelezi
utakapokamilika ili wafikishwe mahakamani. Aliwataja watu hao ambao ni
wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuwa ni Said Ali Abdallah (26),
aliyetoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili
wa Rais na watendaji wa jeshi la polisi.
Alisema mtuhumiwa huyo alitoa maneno hayo na kusambaza vitisho
katika mitandao ya kijamii akisema endapo mwaka huu katika uchaguzi mkuu
CUF haitashinda, watachoma kambi na nyumba za jeshi hilo kisiwani
Pemba.
Alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni Hussein Mageni Hussein, maarufu
Beko (27), ambaye alimpigia simu Balozi Iddi na kumtukana na kumtumia
ujumbe wa simu wenye maneneo ya kashfa.
“Katika ujumbe wa sauti uliokuwa ukisambazwa na mtuhumiwa Said Ali
Abdallah alitoa onyo kwa viongozi wakuu akimtaka rais wa Zanzibar na
makamo wa pili wa rais wasiende Pemba kwani hakuna wafuasi wa chama chao
na kudai kuwa chama anachokishabikia ambacho ni CUF kisiposhinda kwenye
uchaguzi mkuu ujao atahamasisha wafuasi wezake wazitambue nyumba za
askari polisi na waziteketeze familia za askari hao,” alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kisiwani Pemba Mei 20, na
kuonekana kuwa watuhumiwa hao ni wahalifu wa kawaida wasio na msukumo wa
viongozi wa vyama vya siasa katika ushabiki wao.
Alisema baada ya kuwakamata watuhumiwa hao jambo lililowashangaza,
baadhi ya viongozi wa CUF na wanasheria wamekuwa mstari wa mbele
kuwashambilia wahalifu hao.
Alisema baada ya mtuhumiwa Said Ali kufikishwa makao makuu ya
polisi Zanzibar, Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija (CUF),
akiwa na mawakili watatu wa chama hicho walifika na kuanza kumtetea
mtuhumiwa huyo hata kabla hajaanza kuhojiwa.
Alisema hali hiyo inatoa picha kuwa watuhumiwa wanashawishiwa na
viongozi wa CUF wakishirikiana na mawakili ili kuvuruga amani ya nchi.
Alisema uchunguzi wa awali, umebaini kuwa watuhumiwa wametenda makosa
hayo kwani hata mawasiliano ya simu waliyokuwa wakitumia yalichunguzwa
na kujulikana ni wao na maeneo wanayoishi.
“Simu walizokuwa wakitumia ni za mtandao wa Zantel na tulifuatilia hadi katika kampuni ya mtandao huo na tukawabaini,” alisema.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment