RAIS wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Dk Ali Mohamed Shein amewaambia wafuasi wa CCM kwamba
wasihofu, kwani kamwe nchi haiwezi kuondolewa madarakani kwa kufanya
uganga wa kienyeji.
Dk Shein alisema hayo wakati aliposalimiana na wafuasi wao katika
Tawi la Wesha Shengejuu, ambalo ameahidi kulijenga upya baada ya
kuchomwa na watu wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).
Alisema hayo baada ya wafuasi wa CCM, kudai kwamba viongozi wa CUF
wamekuwa wakikesha kucha kutwa wakionekana kwa waganga wa kienyeji kwa
ajili ya kuiroga serikali ing’oke madarakani.
“Mkipata nafasi waambieni wapinzani kwamba nchi haiwezi kuondolewa
madarakani kwa kufanya uganga wa kienyeji na kuroga.....,” alisema Dk
Shein. Alisema uongozi wa nchi unapatikana kwa njia ya kushiriki katika
uchaguzi unaoitishwa na Tume ya Uchaguzi kama ndiyo chombo halali kwa
mujibu wa Katiba chenye majukumu ya aina hiyo.
Alisema kwamba CCM kiliamua kuingia katika kinyang’anyiro cha
uchaguzi wa marudio, ulioitishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
kutokana na kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25. “Hizo ndiyo njia sahihi
ambazo zitamwezesha kiongozi wa nchi kushika dola baada ya kupata ridhaa
kutoka kwa wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi wa marudio,”
alisema Dk Shein.
Hata hivyo, Dk Shein alitoa onyo kali kwa watu wanaofanya matukio ya
vitendo vya hujuma. Alisema kama wapo wanaume, sasa wajitokeze kuvunja
matawi mapya yatakayojengwa. “Natoa onyo kwa watu wanaofanya matukio ya
vitendo vya hujuma kwamba matawi yaliyovunjwa tutayajenga na
watakayavunja basi ole wao watakiona cha moto,” alisema.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment