NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdallah Juma Abdallah “Mabodi” amesema
chama hicho kimejipanga kufanya siasa zenye ushindani wa kisera,
kitaaluma, kiubunifu ili kwenda na wakati wa siasa za kisayansi
zitakazojenga mazingira ya ushindi wa Dola kwa CCM mwaka 2020.
Msimamo huo ameutoa katika Ziara yake ya mwanzo toka akabidhiwe madaraka iliyofanyika Mkoa wa Kusini Unguja, ameeleza kwamba chama kina nyenzo za kila aina zitakazotumika katika uwanja wa kisiasa kwa lengo la kuifuta CUF na vyama vingine vyenye vinavyoshirikiana na chama hicho katika historia ya siasa za Zanzibar.
Mwanasiasa
huyo Mkongwe myenye Taaluma ya Udaktari ameweka wazi kuwa atatumia
falsafa ya Sayansi ya Siasa kufuta kabisa upinzani Visiwani Zanzibar,
kwani vyama hivyo hasa CUF wameshindwa hata kushauri utekelezaji wa
Ilani ya CCM badala yake wanaeneza chuki na misimamo ya utengano kwa
wananchi.
Ameeleza
kwamba Vyama vyenye asili ya migogoro na uchu wa madaraka, haviwezi
kuongoza nchi hivyo jamii iviepuke na wafuasi wa vyama hivyo wahamie CCM
milango ipo wazi ili wanufaike na siasa za maendeleo na demokrasia
imara.
Dkt.
Juma amesema ili kufikia malengo hayo kila mwanachama na mfuasi wa CCM
pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kuimarisha dhana ya umoja na
mshikamano huku wakitafakari njia bora za kuzibakisha madarakani
serikali za CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Pia akizungumza na wanachama wa Tawi la CCM Mtende Mkoani humo amewataka wafuasi
wa chama hicho kufungua ukurasa mpya wa kuanzisha miradi ya maendeleo
katika matawi yao ili waweze kujitegemea wenyewe badala ya kuwa tegemezi
kwa wabunge, wawakilishi na madiwani.
Aliupongeza
uongozi wa Tawi hilo pamoja na Shehia ya Mtende kwa hatua za
kimaendeleo walizofikia katika sekta za miundombinu, afya na elimu na
kuzitaka mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza
changamoto ya upungufu wa maji safi na salama kwani visima vya eneo hilo
vimengia maji ya chumvi.
“ Mtaji wa CCM ni wananchi hasa wale wanaokiamini chama na kukipigia kura kila uchaguzi hivyo nyinyi ndio waajiri
wetu mliotukabidhi majukumu ya kiutendaji na kiuongozi ni lazima
tukutumikieni kwa uadilifu na weledi unaoendana na hadhi ya chama chetu.
Pia nakukumbusheni kuwa maendeleo yanayopatikana hivi sasa yanatokana na radhi za Wazee
wetu ambao ni waasisi wa ASP na TANU ambayo ni CCM ya sasa
inayotutengenezea maisha bora yanayoambatana na amani na utulivu kwa
kila mwananchi.”, Alisema Dkt. Mabodi na kuwasihi Wana CCM kuendelea kuwa karibu na kuwashawishi wafuasi
wa Vyama vya Upinzani kujiunga na Chama hicho ambacho ni kinara wa
Demokrasia, amani, utawala bora na siasa za maendeleo.
Aidha ametoa agizo kwa Wabunge,
Wawakilishi na Madiwani wa Chama hicho kuwasilisha mrejesho wa
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa ngazi husika
kila baada ya miezi mitatu ili kufanyike tathimini za kitaalamu
zitakazopima utekelezaji wa Ilani hiyo kama unaendana na mahitaji ya
wananchi waliyoahidiwa katika Kampeni zilizopita.
Hata hivyo aliagiza kutekelezwa haraka agizo la kila Tawi la CCM katika Mkoa wa Kusini kuwekwa kwa sanduku la maoni ambalo kila mwanachama mwenye kero atatumia njia hiyo kuwasilisha maoni yake moja kwa moja ili Afisi Kuu CCM Zanzibar kwa kutumia utaratibu maalum itayachambua kwa kina kwa lengo la kubaini mambo yanayokwamisha utekelezaji wa ilani kwa baadhi ya maeneo.
Akizungumzia zoezi la Uchaguzi wa
Chama unaoendelea hivi sasa kwa ngazi ya matawi alisema Chama bila kuwa
na Wazee wenye hekima na busara hakiwezi kwenda kwani vijana pekee yao
hawana uwezo wa kuongoza bila ushauri wa Wazee hivyo taasisi hiyo inahitaji mchanganyiko wa makundi yote kugombea nafasi za uongozi hasa ngazi za matawi.
Wakati huo alizindua na kuweka jiwe la Msingi katika Maskani mbali mbali zikiwemo
Maskani ya Haroun, Haji Jecha , Tumegutuka na Maskani ya Kisonge ambapo
jumla ya wanachama wapya 90 kutokana CUF wamejiunga na CCM na
kukabidhiwa kadi rasmi za chama.
Akitoa maneno ya Shukrani Mwakilishi
wa Jimbo la Makunduchi Unguja, Haroun Ali Suleiman aliwambia wanachama
wa chama hicho kuendelea kuiamini na kuiunga mkono CCM ili iweze
kuwaletea maendeleo endelevu huku ikilinda Amani na utulivu wa nchi.
Ziara hiyo ya siku moja yenye lengo la kuimarisha uhai wa Chama na kuongeza hamasa kwa wanachama wa ngazi za Mashina na Matawi ya CCM kuamini kuwa wao ndio nguzo ya mafanikio ya Chama ambapo Viongozi mbali mbali wa chama, serikali na jumuiya wameshiriki katika ziara hiyo.
Viongozi
hao ni pamoja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa kusini, Ramadhani Abdalla
Ali, Katibu wa Mkoa Sauda Mpambalyoto, Mwenyekiti wa Wilaya ya Kusini
Abdulaziz Haji, Mkuu wa Wilaya Kusini Idrissa Kitwana Mustafa na Katibu
wa UVCCM Wilaya ya kusini Haji Mwalimu.
0 comments:
Post a Comment