Home » » WAZIRI WA ULINZI DK EMMANUEL NCHINI ATUA VISIWANI ZANZIBAR NA KUKEMEA VITENDO VYA VURUGU

WAZIRI WA ULINZI DK EMMANUEL NCHINI ATUA VISIWANI ZANZIBAR NA KUKEMEA VITENDO VYA VURUGU

Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar

Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Dk. Emmanuel Nchimbi ametua Visiwani Zanzibar
leo ambapo amekemea vitendo vya vurugu,akiahidi Serikali kuwachukulia
hatua ikibidi hata kuwavizia nje ya misikiti kwa wale watakaohusika na
uvunjifu wa amani .

Waziri Nchi aliwasili Mjini Zanzibar akiwa na Mkuu wa Jeshi  la
Polisi,Inspekta Jenerali Said Mwema kwa pamoja waliitisha mkutano
uliowakutanisha viongozi wa Jumuiya ya Maimamu
Zanzibar(JUMAZA),Mabalozi,Kamisheni ya Utalii, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam Zanzibar(JUMIKI).

“Suala
la kufuata sheria halina mjadala,lazima kila mmoja wetu afuate na kutii
sheria hatutawavumilia watakaovuruga amani ya nchi…maandamano yoyote
lazima yapate kibali” Aliwaambia wadau katika mkutano huo uliofanyika
Makao Makuu ya Polisi Zanzibar,Ziwani.

Waziri
Nchi alisema busara ya Polisi imefikia kikomo na kwamba atashangaa sana
akiona busara hiyo ikiendelea wakati kuna watu au kikundi kinavunja
amani ya nchi.
“Tutashangaa
busara ya Polisi ikiendelea wakati watu wanaumia kwa watu wengine
kuvunja amani…hatutakubali, tutaendelea kuviziana hata nje ya misikiti
tutawakamata” Alisisitiza Waziri Nchi.

Waziri
huyo alisema kila mtu anawajibika kitunza amani iliyopo ambapo pia
alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yenye mfumo wa Umoja wa Kitaifa
imefanyakazi nzuri katika kipindi kifupi na kuwapongeza Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk. Ali Mohammed Shein, Makamu wa
Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad na Makamu wa Pili wa Rais
Balozi Seif Ali Idd.


 “Jamani
Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatufanyia kazi nzuri kwanini mnataka
kuwachafua viongozi wetu,lazima mfuate sheria hakuna mbadala wa hilo
kwani dini zote zinahimiza amani,umoja na mshikamano.

Alisema
Serikali inataka utulivu ndani ya mioyo ya watu na sio utulivu huo
usiishie kuonekana barabarani tu, “watu waishi bila hofu kwa utulivu
kabisa huku mioyo yao ikiwa imetulia” Aliongeza Dk. Nchimbi.

Alitoa
wito kwa viongozi wa dini, vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla
kuwafichua wahalifu wote waliohusika na matukio ya wizi,uporaji wa mali
na uharibifu wa vitu na mali mbalimbali wakati wa matukio ya wiki
iliyopita.

“Wananchi
wafichueni wahalifu ,tusichanganye uislamu na uhalifu” alisisitiza
Waziri Nchi katika mkutano huo ambapo viongozi wa dini waliahidi
kuchukua hatua kusambaza ujumbe wa Waziri huyo kwa waumini na wananchi
wengine kutunza amani na kujieepusha na vurugu.

Katibu
wa JUMAZA,Sheikh Muhidin Zubeir Muhidin alisema Jumuiya yake ni tofauti
na Jumuiya ya Uamsho hivyo watu wasizichanganye. Alisema Maimamu
wataelezana ulazima wa kuwaeleza waumini kufuata na kuzitii sheria sio
tu za Mwenyezimungu bali hata za Serikali.

Katika mkutano huo kulikuwa na wawakilishi wa Balozi za Marekani, Canada, Uingereza na Norway.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa