Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpongeza Balozi Mpya wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Balozi Tavaku Manongi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (katikati) akizungumza na Balozi mpya wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Balozi Tavaku Manongi Nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam. Kushoto ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhan Mwinyi Muombwa.
Balozi mpya wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tavaku Manongi amesema Uongozi wake utajitahidi kuangalia maeneo yanayoigusa Zanzibar moja kwa moja katika jitihada za kunyanyua Uchumi na kustawisha Maendeleo ya Jamii.
Balozi Tavaku akiambatana na Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhan Mwinyi Muombwa ameeeleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi nyumbani kwake Mtaa wa Namanga Mjini Dar es salaam.
Amesema yapo masuala ambayo Zanzibar ina fursa ya kuyafanya na kuyafuatilia bila ya kuathiri yale maeneo ambayo hushughulikiwa moja kwa moja kwa mujibu wa taratibu za Kimuungano.
Balozi Tavaku amesisitiza kwamba utendaji wake mara zote utazingatia zaidi Umoja na Ushirikiano kati yake, Watendaji atakao waongoza pamoja na Taasisi, Jumuiya na Nchi washirika. Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amempongeza Balozi Tavaku kwa kuteuiwa kushika wadhifa huo na kumtaka awe makini katika kupambana na changamoto zitakazomkabili katika utumishi wake huo mpya.
Balozi Seif amemueleza Balozi Tavaku kwamba miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja mchakato wa Tanzania kuelekea katika katiba mpya ambayo tayari Wananchi wameanza kutoa maoni yao.
Alisema yapo matatizo katika katiba ya sasa na kitachozingatiwa zaidi katika fursa ya Wananchi ya utoaji wa maoni ni kuhakikisha kasoro na upungufu uliopo unaondoshwa kwa kujenga katiba madhubuti itakayokidhi mahitaji ya Jamii yote ya Watanzania
0 comments:
Post a Comment