Home » » Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akutana na uongozi wa kampuni ya Transworld ya Dubai

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akutana na uongozi wa kampuni ya Transworld ya Dubai


 Mwenyekiti wa Makampuni ya Transworld yenye Makao yake Dubai Bwana Abdallah Karusi pamoja na Mkuu
Masoko wa Makampuni hayo Mhandisi Adil Abdull Jalil kushoto yake
wakimsikiliza Balozi Seif hayupo pichani wakati wa mazungumzo yao
Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na
Ujumbe wa Kampuni ya Kimataifa ya Transworld yenye Makao Makuu yake
Dubai ukiongozwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya Transworld Bwana Abdallah
Karusi.Mazungumzo hayo
yaliyoshirikisha pia Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mh. Othman Masoud,
Katibu Mkuu wizara ya Nchi Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Nd.
Khamis Mussa, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nd. Mwalimu Ali na Mkurugenzi Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} Nd. Salum Khamis yalifanyika katika ukumbi wa Ofisi yake iliyopo Vuga Mjini Zanzibar
---


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeushauri Uongozi wa Kampuni ya
Kimataifa ya TransWorld yenye Makao Makuu yake Nchini Dubai kuangalia
maeneo ambayo inaweza kuweka Vitega Uchumi vyake hapa Zanzibar.

 
Ushauri huo umetolewa na Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati alipokutana na Ujumbe
wa Kampuni hiyo hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo
unaoongozwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya Transworld ambaye ni mzaliwa
wa Zanzibar Bwana Abdallah Karusi kwamba uwekezaji wa Makampuni hayo
hapa Zanzibar unaweza kusaidia maendeleo na Ustawi wa Jamii wa Wananchi
pamoja na ongezeko la mapato kwa Makampuni hayo.


Alisema kwa vile Kampuni hiyo
inajihushisha na Miradi tofauti ya Kimataifa ni vyema kwa Watalaamu wake
kuja hapa Zanzibar kukutana na Viongozi wa Taasisi husika na baadaye
kuangalia na kuona miradi wanayoweza kuwekeza kwa faida ya pande zote
mbili.
Mapema Meneja Mkuu wa Masoko wa Kampuni
ya Transworld Mhandisi Adil Abdull Jalil alisema Kampuni yao imekuwa
ikijihusisha na miradi ya Miundo mbinu ya Habari na Mawasiliano { IT },
Usafiri wa Anga, Umeme, Mafuta pamoja na Sekta ya Utalii.
Mhandisi Adil Abdul Jalil alisema
Kampuni yao imekuwa na Mashirikiano ya karibu na Makampuni mbali mbali
ya Kimatifa katika Mataifa ya Marekani, Ufaransa, Dubai sambamba na na
eneo la mashariki ya Kati.
Mhandisi Adil aliutaja mradi wa Usafiri
wa anga pekee umefikiwa uwekezaji wa gharama ya zaidi ya Dola za
Kimarekani Milioni Mia Saba { 700,000,000 U$ } miradi inayoendeshwa kwa
takriban miaka 35 sasa tokea kuasisiwa kwa Kampuni hiyo ya Kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Makampuni ya Transworld Bwana Abdallah Karusi aliisifu Zanzibar na Kubarikiwa kuwa na mazingira mazuri katika miradi ya Uwekezaji Vitega Uchumi.
Bwana Abdalla alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba uwezo wa kuifanya Sekta
ya Mawasiliano kuwa ya Kimataifa zaidi inawezekana iwapo Uongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utashirikiana na Makampuni yanayonia
ya kutaka kuwekeza Nchini.
Mkutano huo pia ulishirikisha
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Othman Masoud
Othman, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Nchi Fedha, Uchumi na Mipango ya
Maendeleo Nd. Khamis Mussa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi maendeleo ya
Makazi, Maji na Nishati Nd. Mwalimu Ali Mwalimu na Mkurugenzi wa Taasisi
ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar { ZIPA } Ndugu Salum Khamis.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliangalia
harakati za ukatwaji wa muembe katika eneo la Magomeni ambao ulikuwa
ukilalamikiwa na Wakaazi wa eneo hilo kwamba ulikuwa katika mazingira hatarishi kutokana na waya wa umeme uliokuwa chini ya matawi yake.
Katika ziara hiyo Balozi Seif aliwaka
Viongozi wa Taasisi zinazohusika na maamuzi kuchukuwa hatua mara moja
mara tuu linapotokezea tatizo badala ya kusubiri malalamiko kutoka kwa
Wananchi.
Hata hivyo Balozi Seif
aliwatahadharisha Wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya pembezoni
mwa Bara bara kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya Biashara ambavyo
baadaye huleta usumbufu wakati wa upanuzi wa bara bara.

Na 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa