na Mwandishi wetu, Zanzibar
LIGI
Kuu ya soka ya Grand Malt ya visiwani hapa, iliendelea juzi kwa timu ya Bandari
kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mundu kwenye Uwanja wa Amaan.
Katika
mchezo huo uliokuwa na ushindani pande zote mbili karibu muda wote, ilikuwa ni
dakika ya 42, Bandari walipofanikiwa kupata bao pekee kupitia kwa mshambuliaji
wake, Hissam Hamis.
Hata
hivyo, washambuliaji wa Mundu hawakuwa makini, kutokana na kupoteza nafasi
kadhaa walizotengeneza na kuishia kupiga mashuti pembeni ya lango na
kusababisha wapoteze pointi tatu muhimu kwenye ligi hiyo.
Katika
mchezo mwingine uliofanyika Pemba, kwenye dimba la Gombani, mabingwa wa zamani
wa ligi hiyo, Jamhuri, waligawana pointi na Mtende ambayo imepanda daraja msimu
huu, baada ya dakika 90 kumalizika wakiwa sare ya bao 1-1.
Ligi
hiyo ilitarajiwa kuendelea tena jana jioni, kwa kuzikutanisha timu za Malindi
na Chuoni kwenye Uwanja wa Amaan, wakati huko Pemba, Chipukizi watawakaribisha
maafande wa Mafunzo Uwanja wa Gombani na leo jioni, Dume itavaana na Mtende
huku usiku Falcon watachuana na Mafunzo.
Kampuni
ya Bia Tanzania kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha Grand Malt, ndio
wadhamini wakuu wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 12 kutoka Unguja na Pemba.
Mshindi
wa kwanza wa ligi hiyo ataiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya Klabu Bingwa
Afrika pamoja na michuano ya Kombe la Kagame huku mshindi wa pili atapeperusha
bendera ya Zanzibar kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho (CAF).
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment