Home » » BUTOYI AWAGAWA VIONGOZI SIMBA

BUTOYI AWAGAWA VIONGOZI SIMBA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

Ujio wa beki mpya wa Simba, Mrundi Butoyi Hussein umewagawa viongozi wa Simba katika makundi mawili yanayopingana juu ya usajili wake, ingawa kocha Patrick Phiri amesema aachiwe kazi hiyo aifanye mwenyewe.
Butoyi yupo visiwani hapa akifanya majaribio, ambapo viongozi wengi hasa kutoka kundi lenye ushawishi mkubwa la Friends of Simba wakihitaji beki huyo asajiliwe huku wakitaka Mkenya Donald Mosoti aondolewe katika kikosi chao kama alivyoomba hapo awali kuvunja mkataba wake.
Hata hivyo, Phiri amekuwa mgumu wa kutoa uamuzi wake juu ya wachezaji wake hao wawili Mosoti na Butoyi ingawa ni lazima mmoja wao aondoke kwani sheria za usajili wa wachezaji wa kigeni zinahitaji kila timu iwe na wachezaji watano tu wa kigeni.
Tayari Simba ina wachezaji wake watano wa kigeni ambao ni Mganda Joseph Owino, Mkenya Raphael Kiongera, Warundi Amissi Tambwe na Pierre Kwizera pamoja na Mosoti mwenye mkataba wa mwaka mmoja na nusu kwani alisajiliwa dirisha dogo msimu uliopita.
Kazi ya kumsaka beki huyo kutoka timu ya Telecom ya Djibouti ilifanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zacharia Hans Poppe aliyefunga safari mpaka Kigali yalikokuwa yakifanyika mashindano ya Kombe la Kagame baada ya Kamati hiyo kujadili na kukubaliana kwa pamoja kuwa atafutwe beki mwingine haraka ili Mosoti aruhusiwe.
Jana Jumapili Simba ilicheza mechi yake ya kirafiki dhidi ya Kilimani City, mechi iliyochezwa Uwanja wa Amaan na kuhudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Simba kwa lengo la kuangalia kiwango cha Butoyi.
“Tutamsikiliza kocha (Phiri) anasemaje, lakini tumeangalia kwa umakini uamuzi wa Mosoti wa kutaka kuondoka, si hilo tu hata kiwango chake ndio maana tunataka kufanya marekebisho kabla ligi haijaanza, hivyo uwezekano wa kumsajili Butoyi ni mkubwa ili kumpa nafasi Mosoti ya kwenda anakotaka,” alisema kiongozi mmoja wa Friends of Simba, hata hivyo baadhi ya wajumbe wa kamati ya usajili na kamati ya utendaji ya Simba walipinga uamuzi huo kwa madai kuwa Mosoti anatakiwa kupewa muda mpaka wakati wa dirisha dogo.
Mosoti aliliambia gazeti hili kuwa,“Kama nilivyosema awali kuwa nilizungumza na viongozi wangu juu ya kuondoka, lakini pia sioni kama kutakuwa na tatizo nikiondoka kwani wachezaji waliopo Simba ni wazuri na wataisadia Simba kwa kiasi kikubwa tu.”
Kuhusu mkanganyiko wa wachezaji hao wawili, kocha Phiri alisema, “Baada ya mechi kadhaa ndipo nitakuwa na jambo lolote la kuzungumzia kuhusiana na wachezaji hao, kwani kwa muda niliokaa nao mazoezini wote ni wazuri ila siwezi kuwapima kwa njia ya mazoezi pekee.”
Wakati huohuo, kiungo mpya wa Simba Mrundi, Pierre Kwizera amesema kila nafasi katika kikosi chao kuna changamoto ya kupata namba kwani timu ina wachezaji wengi ambao ni wazuri.
Kwizera alisema tangu kocha Phiri ametua Simba kumekuwapo na mabadiliko makubwa katika kikosi chao kwani wachezaji wanaonyesha viwango vya juu mazoezini.
 Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa