Home » » UCHUNGUZI WA KOMPYUTA WAKAMILIKA

UCHUNGUZI WA KOMPYUTA WAKAMILIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
Jeshi la Polisi Zanzibar, limesema kazi ya kuchunguza kompyuta mpakato ya waziri wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, (SMZ), Mansoor Yussuf Himid, aliyefunguliwa mashtaka matatu yakiwamo ya kukamatwa na silaha ya moto na risasi 407, imekamilika.
Hata hivyo, limesema kuwa hakuna kitu kibaya kilichokutwa ndani yake.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi jana, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Kamishna Msaidizi wa Polisi (DDCI), Salum Msangi, alisema kuwa kazi ya kuchunguza kompyuta hiyo imefanyika kwa umakini mkubwa na wataalamu wa mawasiliano ya mitandao wa jeshi hilo.
“Hakuna kitu kibaya tulichofanikiwa kukamata baada ya kukamilika kwa uchunguzi wake,”alisema DDCI Msangi.
Hata hivyo, alisema kwamba baada ya kuifungua na kufanya upekuzi katika mfumo wa mtandao wa mawasiliano wa kompyuta hiyo hakuna kitu chochote cha jinai walichogundua zaidi ya mawasiliano yake binafsi.
Akifafanua zaidi alisema kwamba kazi ya mwisho inayoendelea kufanywa na maofisa wa upelelezi ni kukamilisha ushahidi katika kesi ya msingi na wakati wowote Mansoor atarejeshewa kompyuta yake.
Kompyuta hiyo ilichukuliwa na polisi kwa uchunguzi baada ya Mansoor kupekuliwa nyumbani kwake Chukwani Agosti 2 mwaka huu, ambapo alipatikana na silaha ya moto na risasi 407, kinyume na Sheria ya Silaha na Risasi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, DDCI Msangi alisema kwamba upelelezi wa kesi bado haujakamilika, licha ya mshtakiwa kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka matatu.
Kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Agosti 28 mwaka huu.
Waziri huyo wa zamani yupo nje kwa kwa dhamana ya masharti ya kutosafiri nje ya Zanzibar bila ya ruhusa ya mahakama, kusalimisha hati ya kusafiria, pamoja na wadhamini wawili kwa bodi ya shilingi milioni tano kila mmoja na fedha taslimu shilingi milioni tatu
  Chanzo;Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa