Kumekuwa na Taarifa potofu zinazosambazwa na baadhi ya watu
katika mitandao ya kijamii ya kuwa “Mwanasheria
Mkuu Zanzibar Othman Masoud Othman amekamatwa
baada ya kupiga kura ya hapana Bungeni leo”
Tunapenda kuutarifu Umma wa Watanzania kuwa, taarifa hizo
sio sahihi na ni porojo zenye kutaka kuleta hisia potofu kwa wananchi kuhusu
kiongozi huyo.
Ukweli wa Jambo hili ni
kuwa Mhe. Othman Masoud Othman ametekeleza
haki yake ya Kidemokrasia ya kupigia
kura Rasimu ya Katiba inayopendekeza katika Bunge Maalum leo. Ambapo katika kura alizopiga, ameweza kuzikubali
baadhi Ibara na kuzikataa ibara nyingine katika rasimu ya Katiba
inayopendekezwa.
Pengine hatua hiyo ya kuzikataa baadhi ya Ibara,
haikuwafurahisha baadhi ya Wajumbe na hivyo kuleta majibishano ndani ya Bunge
Maalum wakilalamikia uamuzi wake huo.
Kutokana na hofu hiyo ya baadhi ya Wajumbe kuanza kupinga
uamuzi wake huo ndani ya Bunge, Ofisi ya Bunge Maalum kama ilivyokawaida kwa
kila mjumbe, imeweza kumpatia Ulinzi Maalum wakati akitoka Bungeni hadi
alipoondoka katika viwanja vya Bunge ili asiweze kubugudhiwa kwa namna yoyote
ile kutokana na uamuzi wake huo.
Suala hili limechukuliwa kipropaganda na kuanza kueneza
uongo katika mitandao ya kijamii kuwa Mhe. Othman amekamatwa baada ya kupiga
kura ya hapana.
Tunapenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa Mhe. Othman
hajakamatwa bali alipewa ulinzi katika Maeneo ya Bunge Maalum jambo ambalo
hufanyika kwa kila mjumbe ambaye kwa namna moja ama nyingine itaonekana kuna
dalili za kubugudhiwa katika Maeneo ya Bunge kutokana na uamuzi au kitendo
alichofanya. Na kutokana na hali ilivyo, ulinzi wake umeimarishwa pia mahali alipo
kwa hivi sasa mpaka atakapomaliza kazi yake hapa Dodoma.
Kanuni za Bunge Maalum zimempa madaraka Katibu wa Bunge
Maalum kusimamia masuala yote ya Ulinzi na Usalama kwa Wajumbe na Maeneo yote
ya Bunge Maalum.
Imetolewa na Idara ya Habari
Ofisi ya Bunge Maalum
Dodoma
1 Oktoba, 2014
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment