Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif
Hamad, amemwangukia Papa Benedict XVI kwa kumwandikia barua, akimuomba
kutumia ushawishi wake na Tanzania kumaliza mzozo wa kisiasa kisiwani
humo kabla hali haijawa mbaya.
Kwa mujibu wa barua yake ya Novemba 25, mwaka jana ambayo gazeti
hili imefanikiwa kuona nakala yake, Maalim Seif alimwomba Papa kutumia
ushawishi alionao kwa serikali ya Tanzania ili kuhakikisha haki
inatendeka na kuepusha vurugu zinazoweza kutokea.
“Ni wiki tatu sasa tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu na hali hii
imesababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli za kuichumi kutokana na
wananchi wengi kuwa na hofu kuhusu mustakabali wa hali hii….watu
wanashindwa kujua nini kitatokea maana wana hofu kwamba hali hii inaweza
kuharibu umoja wa kitaifa kwa watu kuishi kwa upendo bila kujali dini
wala kabila,” ilisema barua hiyo.
Barua hiyo ya Maalim Seif ilisema, Zanzibar ina mchanganyiko wa
Waislamu na Wakristo, hivyo hakuna mgawanyiko kwa misingi ya udini
lakini hatua ya wananchi kukosa haki yao ya kidemokrasia kupitia sanduku
la kura baada ya miaka 20 ya chaguzi visiwani humo kunaweza kusababisha
vijana ambao hawafurahishwi na mwenendo huo kutumia njia mbaya kutafuta
haki yao.
“Badala ya kuchukua hatua za pamoja kuzuia uovu huu, Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo chama chake kilishinda kwenye
uchaguzi mkuu uliopita, imekuwa ikisaidia serikali ya Zanzibar kwa
kutumia askari na majeshi yake kutishia watu wa upinzani,” ilisema.
“Wakati mmishenari wa kikristu alipomuomba Sultan wa Zanzibar
mwaka 1840 kibali cha kujenga asasi ya kusaidia jamii kwenye eneo
lake, Sultani yule ambaye alikuwa Muislamu alimtambua kama mtumishi wa
Mungu aliyekuwa na lengo la kuendeleza neno la Mungu” ilisema sehemu ya
barua hiyo kwenda kwa Papa.
Iliongeza kuwa, Zanzibar ilipopata Uhuru wake mwaka 1963, kwa
kiwango kikubwa watu wake waliishi kwa amani na ushirikiano baina ya
watu wa madhehebu yote ya Katoliki, Anglikana, Sunni, Shia na Hindu na
hakukuwahi kuwa na mgogoro wala hofu ya watu hao kuhitilafiana kwa
misingi ya tofauti ya dini.
Ilisema Chama cha Wananchi CUF kimekuwa kikishinda chaguzi zote
tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, lakini haijawahi
kupewa ushindi wake hata muhula mmoja.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment