Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimewataka viongozi na watendaji wa chama hicho kuhakikisha mikataba ya
kibiashara wanayofunga inapitiwa na kuwashirikisha wanasheria ili
kuepuka vitendo vya utapeli.
Kimesema
kuwashirikisha wanasheria wakati wa kufunga mikataba ya aina mbali
mbali ya kukodisha Mali za Chama hicho kutasaidia kumaliza kero na
migogoro ya matumizi mabaya ya Rasilimali za CCM.
Hayo aliyasema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai katika mwendelezo wa ziara ya kukagua na kuhakiki mali za Chama hicho huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema matatizo ya matumizi mabaya ya Mali za chama hicho yanayojitokeza katika maeneo nchini ni kutokana na
baadhi ya viongozi na watendaji kufunga mikataba ama makubaliano na
wafanyabiashara bila ya kuwashirikisha wanasheria ama kupata ushauri
kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu hali inayopelekea baadhi ya watu kutumia nafasi hiyo kujinufaisha wenyewe badala ya kuangalia maslahi ya CCM.
Vuai
alieleza kwamba njia pekee ya kuziweka salama mali mbali mbali za chama
hicho ni uwepo wa maridhiano na makubaliano yanayojali na kuzingatia
matakwa ya kisheria.
“
Naendelea kusisitiza kwamba mali za CCM hazipo kwa ajili ya
kuwanufaisha watu wachache, bali zipo kwa ajili ya kukinufaisha chama
ambacho ni taasisi halali ya watu wengi na jambo lolote la umiliki wa
Rasilimali zake lazima liendeshwe kwa misingi ya uwazi na usawa kupitia
utaratibu halali wa kisheria.
Pia
Mali zote kwa sasa ni lazima zitumike ipasavyo kwa mujibu wa matakwa ya
sera ya CCM ya siasa kwenda sambamba na ukuaji wa uchumi ndani ya chama
chetu.”, alisisitiza Vuai na kuongeza kuwa CCM kwa sasa inaendelea na
mipango ya kuhakikisha Rasilimali zake zinatumika vizuri kuimarisha
uchumi wa Chama hicho badala ya watu wachache wanaojimilikisha mali hizo
kinyume na taratibu.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuhakiki mali za Chama hicho pamoja na kuwakumbusha Viongozi
na Watendaji wa Chama na Jumuiya kwamba chombo pekee kinachomiliki mali
zote ni Baraza la Wadhamini la Chama hicho hivyo hakuna chombo kingine tofauti na baraza hilo kinachoweza kutoa maamuzi ya kuuza mali za Chama.
Aliwaagiza
Viongozi wa Mkoa huo kupitia upya mikataba yote waliyofunga na
wafanyabiashara katika eneo linalomilikiwa na CCM ili kuhakikisha
maslahi yanayopatikana yanaendana na mahitaji ya wakati uliopo sasa
kibiashara.
Aliwasihi
Wana CCM kuendelea na utamaduni wa kuwashirikisha viongozi wa ngazi
mbali mbali za chama hicho pindi panapotokea kasoro za kiutendaji ili
ziweze kutatuliwa kwa kufuata utaratibu wa kinanuni na kimaadili kwa
lengo la kuepuka kauli na malalamiko yasiyofaa ndani ya Chama hicho.
Naibu
Katibu Mkuu huyo alisema kazi iliyopo sasa mbele ya CCM ni kuendelea
kujiimarisha kisiasa huku ikitekeleza ilani ya Uchaguzi ya Mwaka
2015/2020 kwa kasi na kwa ufanisi zaidi ili wananchi waendelee kuiunga
mkono na hatimaye Chama hicho kiweze kuandika historia mpya ya ushindi
wa mwaka 2020.
Alisema
maeneo ya CCM yaliyopo Nungwi ni Rasilimali kubwa kwani yapo katika
ukanda wa Utalii hivyo yanatakiwa kulindwa na kuangaliwa vizuri na
wahusika yasije yakaangukiwa mikononi kwa watu ambalo ni matapeli na
wapinga maendeleo na wakatumia fursa hiyo kupandikiza migogoro na mipasuko isiyokuwa ya lazima ndani ya Chama.
Pamoja
na hayo alisema endapo uongozi wa Mkoa huo utahitaji msaada wa kisheria
Afisi kuu ipo tayari kuwaunga mkono kwa kuwapa mwanasheria wake ili
aweze kuwashauri na kuwaelekeza njia bora ya kufunga mikataba rasmi
inayotambulikana kisheria.
Nao Viongozi
wa Mkoa huo wameahidi kuzifanyia kazi kwa haraka changamoto
zilizojitokeza katika maeneo yanayomilikiwa na chama hicho ili kwenda
sambamba na matakwa ya sera ya ukuaji wa uchumi ya CCM.
Walisema
licha ya CCM ndani ya mkoa huo kuendelea na harakati za kuimarisha
shughuli za kisiasa, bado wana fursa ya kuhakikisha rasilimali za chama
hicho hasa zilizopo katika maeneo ya uwekezaji katika sekta ya utalii
zinakinufaisha chama badala ya watu wachache wanaojali maslahi binafsi.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment