Na Is-haka Omar, Zanzibar.
JUMUIYA
ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekishauri Chama hicho kuiambia
serikali iongeze nguvu katika kusimamia na kudhibiti vitendo vya
udhalilishaji wa Kijinsia wanavyofanyiwa Watoto na Wanawake ili watu
wanaobainika kuhusika na matukio hayo wahukumiwe kisheria kwa mujibu wa
ukubwa wa matukio wanayofanya.
Ushauri
huo umetolewa na Katibu msaidizi idara ya Organazesheni ya Jumuiya
hiyo, Simba Haji Mcha wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kazi
za jumuiya katika mwendelezo wa ziara ya Idara ya Organazesheni Afisi
kuu ya CCM Zanzibar iliyofanyika katika Afisi za Jumuiya hiyo Kikwajuni
Mjini hapa.
Katibu
huyo alivitaja vitendo kuwa ni pamoja na ubakaji, kulawiti, kunajisi na
kupigwa na kutelekezwa kwa watoto na wanawake na kudai kuwa ni aibu
kubwa kwa nchi ya Zanzibar yenye historia na sifa nzuri juu ya maadili
na utamaduni wake mbele ya mataifa mengine.
Alisema
Wananchi wamechoshwa na kufanyika kwa matukio hayo kila mara huku
wahusika wa vitendo hivyo viovu hawachukuliwi hatua zinazostahiki kwa
visingizio vya kutokamilika kwa ushahidi ama kupatiwa adhabu ndogo
isiyolingana na ukubwa wa tukio husika.
Alieleza
kwamba sio tu vitendo hivyo vinatia aibu nchi peke yake bali
vinachangia kuharibu sifa za Chama na serikali kwa ujumla hivyo taasisi
husika waongeze juhudi katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu juu ya
kutatua tatizo hilo.
Katika
taarifa hiyo, Katibu Simba alisema majukumu waliyopewa watekeleze
kikanuni kuwa ni kusimamia suala la elimu, malezi, utamaduni, mazingira
na uchumi mambo aliyoyaeleza kuwa yanayotekelezwa kwa ufanisi mkubwa
kwa lengo la kujenga jamii itakayoweza kukabiliana na kutatua changamoto
mbali mbali za kimaisha.
“
Hali ya kisiasa ndani ya Jumuiya yetu ipo licha ya kuwepo na changamoto
kadhaa zinazotafutiwa ufumbuzi kupitia vikao maalum vya afisi yetu kwa
kufanya tathimini maelekezo ya utekelezaji wa majukumu ya jumuiya na
mambo yote ya kuwahimiza watendaji wa mikoa na wilaya kusimamia jumuiya
kwa mujibu wa kanuni na maelekezo yanayotoka chamani na makao makuu
jumuiya yetu.”, alifafanua Simba.
Alisema
katika kusimamia elimu kwa watoto ili wawe na misingi imara ya
kitaaluma jumuiya inamiliki na kusimamia Vituo vya Chekechea pamoja na
shule mbili za Sekondari na ufundi za Dole Unguja na Dodeani iliyopo
Pemba, ambazo wanafunzi wake wamekuwa wakifaulu kwa kiwango kizuri.
Ameeleza
kuwa kwa upande wa suala la malezi na utamaduni jumuiya imekuwa karibu
na Wazazi na Walezi katika kuhamasisha na kuelekezana juu ya umuhimu wa
malezi bora na athari ya mporomoko wa maadili katika jamii.
Pamoja
na hayo alifafanua kuwa jumuiya hiyo katika suala la kusimamia
Mazingira imekuwa kuhamasisha upandaji wa miti na kupiga vita vitendo
vya uharibifu wa Mazingira vikiwemo uchimbaji wa mchanga holela na
kukata miti ovyo hali inayosababisha ongezeko la athari za tabia nchi.
Akizungumza
Katibu wa Kamati Maalum ya Idara ya Organazesheni Afisi Kuu Zanzibar,
Haji Mkema alieleza kuridhishwa kwake na utendaji na usimamizi wa
majukumu mbali mbali ya kiutengaji na kiuongozi yaliyotekelezwa na
jumuiya hiyo.
Aliikumbusha
jumuiya hiyo kuwa ndio chombo kinachobeba na kulea wanachama wa rika
mbalimbali hivyo wanatakiwa kutambua kuwa uhai wa Chama na jumuiya
unaanzia kwa wanachama wenyewe.
Alisema
lengo la ziara hiyo ni kukutana na Viongozi na Watendaji wa jumuiya
hiyo ili kuwashukru, kubadilishana mawazo na kuona hali halisi ya
utekelezaji wa shughuli za jumuiya na chama kwa ujumla.
“
Nyinyi ndio Wazazi na Walezi wetu na hao Akina Baba, Akina Mama,
Vijana na Watoto wote wapo chini ya malezi yenu hivyo mnatakiwa
kuendelea kuwa mfano bora wa kusimamia kwa vitendo maslahi ya CCM ili
tuendee kushinda kila uchaguzi na kushika dola”., alisema Mkema.
Aliitaka
jumuiya hiyo kuhakikisha takwimu za wanachama wa jumuiya zinakuwa
sahihi na zenye uhalisia ili kuwa na idadi halisi za wanachama halali
watakaosimamia kazi na majukumu ya jumuiya na chama bila ya kuchoka.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Zanzibar, Nagma Murtaza Giga
aliipongeza Afisi kuu CCM kwa ushirikiano wao mzuri na jumuiya hiyo
hatua inayoongeza kasi za kiutendaji kwa lengo la kufanikisha kikamilifu
majukumu ya kisiasa ndani na nje ya Chama.
Giga
alikiomba Chama kusaidia kutatua Changamoto zinazoikabili jumuiya hiyo
katika suala la uendeshaji wa miradi ya jumuiya iliyopo Zanzibar, kwa
lengo la kuhakisha wanatekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2015/2020 inayohimiza falsafa ya siasa na uchumi ndani ya Chama na
Jumuiya.
Aidha
aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli
pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kasi ya usimamizi
mzuri wa shughuli za kiutendaji ndani ya chama na katika serikali
wanazoziongoza ambazo zimezaa matunda yanayowanufaisha wananchi.
Kwa
upande wao Watendaji na Viongozi mbali mbali wa jumuiya hiyo
wanaofanyia kazi Zanzibar, kwa nyakati tofauti wamekiomba Chama vitendo
vya udanganyifu na rushwa katika Uchaguzi wa Chama na jumuiya unaorajiwa
kufanyika mwaka 2017, ili kupata viongozi makini na wenye maadili mema.
Aidha
wamelalamikia suala la kuchelewa kwa utekelezaji wa baadhi ya mambo
yanayojadiliwa katika vikao vya jumuiya hiyo ambayo hawapati mrejesho
wake kwa wakati kutoka Makao Makuu ya Jumuiya, jambo linalochangia
kukwama kwa baadhi ya shughuli za kitaasisi.
Wakati
huo huo, Katibu Mkema alitembelea na kukagua miradi ya jumuiya hiyo
ambayo ni Shule ya Sekondari na Ufundi pamoja na Chekechea zilizopo
katika Kijiji Cha Dole na kuona shughuli za uendeshaji wa miradi hiyo.
0 comments:
Post a Comment