NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.
Chama
Cha Mapinduzi kimewataka Watumishi wake kuelekeza nguvu zaidi katika
kutekeleza ipasavyo majukumu yao kwa weledi na juhudi kubwa ili
kukiletea ufanisi ndani ya Chama hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Mhe. Vuai Ali Vuai, ametoa kauli hiyo, alipokuwa akifungua mafunzo maalum ya
watumishi wa Chama na Jumuiya zake wa kada ya Udereva, Walinzi,
Waangalizi wa Ofisi, Makarani wa Masjala na Wahudumu wa Chama hicho,
kutoka Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar. Mafunzo hayo ya takriban wiki
moja yanafanyika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, Mjini Unguja.
Amesema Chama Cha Mapinduzi kinaridhishwa na utendaji wa watumishi wa kada hizo, isipokuwa CCM
kimeona kuna umuhimu wa kuandaa mafunzo maalum kwa watumishi hao, kwa
lengo la kuwajengea uwezo na uelewa mpana zaidi katika kufanikisha
majukumu yao na hivyo waendane na kasi ya Chama kwa sasa.
Mhe.
Vuai amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwapatia mafunzo
watumishi wake wa kada mbali mbali kwa lengo sio tu la kuwaleta ufanisi
katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya Chama bali pia kuwajengea
uwezo na kuwapa mbinu mbadala za kiutumishi.
“Chama
Cha Mapinduzi kitafanya kila linalowezeka kuhakikisha watumishi wake wa
ngazi zote wanapatiwa mafunzo pamoja na kuwaendeleza kielimu, kwa
madhumuni ya kunyanyua viwango vyao vya uelewa, na hivyo kuweza kufanya
kazi zao kwa ufanisi zaidi”. Alidai Mhe. Vuai.
Amesisitiza
haja kwa wanafunzo hao juu ya umuhimu wa kuimarisha Chama na kudumisha
suala zima la nidhamu pamoja na kuwepo kwa mawasiliano mazuri baina yao
na Viongozi wao, ni dhahiri kutakijengea heshima kubwa chama hicho
mbele ya jamii.
Nao
wanafunzo hao, wametumia mkutano huo kumpongeza kwa dhati Mwenyekiti wa
CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli, kwa jinsi anavyotekeleza kwa kasi kubwa Ilani ya CCM ya mwaka
2015 - 2020 pamoja na kupambana vilivyo na suala zima la rushwa, wizi na
ubadhirifu wa mali ya umma, kwa maslahi ya Taifa na wananchi wake.
Wamempongeza
pia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kusimamia vyema
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 - 2020, kusimamia suala
zima la amani na utulivu wa nchi, kuimarisha huduma za kijamii na
miundombinu ya kiuchumi kwa maslahi ya Wananchi wa Zanzibar.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment