Home » » TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA IKULU YA ZANZIBAR

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA IKULU YA ZANZIBAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 




RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza umuhimu wa viongozi katika Ofisi na Idara za Serikali kuwa na utaratibu wa kufanya mikutano  mara kwa mara na watendaji wao ili kuzungumza na kujadili masuala yao ya kazi.

Dk. Shein aliyasema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujua matatizo ya watendaji wao pamoja na kukaa kwa pamoja kwa lengo la kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo kwa haraka na hatimae kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar katika kikao maalum kati yake na uongozi wa Ofisi ya Rais, na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wakati ilipowasilisha Taarifa  ya  Utekelezaji wa Mpango Kazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba katika Bajeti ya mwaka 2016-2017 ya Ofisi hiyo.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa ni jukumu kwa kila mkuu wa Idara kuwa na utaratibu huo kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kupata maamuzi ya haraka sambamba na kuweza kufanya kazi kwa pamoja hatua ambayo pia, hupunguza mivutano na hujenga mafahamiano makubwa.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa kukaa pamoja kati ya kiongozi na watendaji wake kunasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia muwafaka katika kujadili masuala mbali mbali ya kiutendaji hali ambayo huzidisha mshikamano na kujenga udugu miongoni mwao.

Alisema kuwa hata vikao vya taarifa za Mpango  Kazi wa Mawizara vinavyofanyika Ikulu Zanzibar vimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuyapatia ufumbuzi wa haraka masuala mbali mbali ambayo yameweza kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa.

Alisisitiza kuwa hatua hiyo haitopunguza ama kuondoa heshima kwa kiongozi na badala yake itazidi kujenga heshima na mashirikiano ya karibu miongonimwao badala ya watendaji kumuogopa kiongozi wao.

Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa  Ofisi ya Faragha ya Rais kuwa na utaratibu wa kukutana mara kwa mara na watendaji na kujadili masuala mbali mbali ya kazi zao ambao ulipongezwa katika kikao hicho.

Aidha, Dk. Shein  alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa utendaji wao wa kazi sambamba na kazi nzuri ya uwasilishaji na utekelezaji  wa Mpango Kazi uliofanywa na Ofisi hiyo.

Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee nae alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Ofisi hiyo na kuwataka viongozi na watendaji wake kuwa kioo kwa watendaji na viongozi wa Wizara nyengine za Serikali sambamba na kuionesha vyema taswira ya Rais.

Kwa upande wao, Washauri wa Rais walitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi na watendaji wa Ofisi hiyo kwa kuendeleza ushirikiano na mshikamano katika utendaji wa kazi zao huku wakieleza umuhimu wa ziara za Pemba kwa viongozi wa Ofisi hiyo.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,  Issa Haji Ussi Gavu akisoma  taarifa ya Mpango Kazi wa Ofisi hiyo, na kusema kuwa Ofisi ya Rais imedhamiria kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar ili waishi kwa amani, mshikamano na upendo miongoni mwao.

Alisema kuwa dhamira hiyo itafikiwa kwa kuhakikisha kwamba kunakuwa na mawasiliano ya karibu baina ya wananchi na Mheshimiwa Rais, hali ambayo itaifanya jamii kuwa na imani na Serikali yao na itapelekea kuimarika kwa amani, umoja na mshikamano.

Aidha, alisema kuwa Ofisi itahakikisha kuwa Zanzibar inanufaika na uhusiano wa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kama ilivyosisitizwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015-2020.

Alieleza kuwa Ofisi hiyo itahakikisha kuwa Idara inayoshughulikia masuala ya Diaspora inaimarishwa kwa kuwa na watendaji wenye uwezo na kuweka mazingira mazuri kutendea kazi ambapo pia uongozi wa Ofisi hiyo ulieleza juhudi zinazochukuliwa katika ujenzi na ukarabati wa majengo ya Ikulu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa