Na Is-haka Omar, Zanzibar.
ZAIDI
ya shilingi milioni 43 zimetumika kununua vifaa mbali mbali vya Jimbo
la Chumbuni Zanzibar, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na
Viongozi wa jimbo hilo kwa wananchi katika Kampeni za Uchaguzi
uliopita.
Akisoma
Risala katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, Abrahman Abass
alisema vifaa hivyo vimetolewa na viongozi wa jimbo hilo ambao ni
Mbunge, Mwakilishi na Madiwani.
Alivitaja
vifaa vilivyotolewa kuwa ni Gari moja aina ya Canter, Dawa za binadamu
kwa ajili ya vituo vya Afya vya jimbo hilo pamoja na jezi za mpira wa
miguu kwa timu za jimbo zenye usajili wa ZFA.
Alisema
tangu viongozi hao waingie madarakani kwa kipindi cha miezi 14 kwa
mbunge na miezi minane kwa Mwakilishi na Madiwani tayari wameshatumia
zaidi ya milioni 205 katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ndani ya
jimbo hilo.
Akikabidhi
vifaa hivyo kwa wananchi mbali mbali wa Chumbuni, Naibu Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Vuai Ali Vuai aliwasihi wafuasi wa
Chama hicho na wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi za maendeleo
zinazofanywa na viongozi hao.
Alisema
endapo wananchi wa Jimbo la Chumbuni wataendelea kushirikiana na
viongozi wao vizuri jimbo hilo litakuwa miongoni mwa majimbo ya kuigwa
kimaendeleo hapa nchini.
Vuai
ambaye pia ni Mlezi wa Jimbo hilo alisema Chama hicho kwa sasa
kinahitaji viongozi imara na wabunifu wenye uwezo wa kutekeleza kwa
vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 bila ya kusukumwa
kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“
Suala la maendeleo halina Chama wala kabila kwani misaada inayotolewa
na viongozi wetu wa jimbo hili na mengine naamini wanaonufaika ni
wananchi wote na sio Wana CCM pekee, hivyo tuwaunge mkono juhudi zao na
kuthamini na kutunza vifaa wanavyotoa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
Pia
wananchi nakukumbusheni kuwa juhudi hizi ni matunda ya Mapinduzi ya
mwaka 1964 yaliyofanywa na wazee wetu kwa lengo la kutuweka huru ili
tujitawale na kutengeneza miundombibu imara ya maendeleo ya nchi
yetu.”, alifafanua Vuai na kuwataka viongozi hao kuendelea kutoa
misaada mbali mbali ya kimaendeleo kadri hali za kiuchumi
zitakavyoruhusu ili wananchi waweze kunufaika na fursa hizo.
Aidha
alipongeza viongozi hao kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kwa
wananchi na kuongeza kuwa wametekeleza kwa vitendo matakwa ya Katiba ya
CCM.
Hata
hivyo aliwasihi vijana, wanawake na wazee wa jimbo hilo kujitokeza kwa
wingi katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar
yaliyofanyika mwaka 1964.
Pamoja
na hayo alitoa ahadi ya shilingi milioni moja kwa Vikundi mbali mbali
vya ujasiriamali vya jimbo hilo ili ziweze kuwasaidia katika harakati
zao za kimaendeleo.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo hilo, Ussi Salum Pondeza “Amjadi” alisifu
ushirikiano uliopo baina yake na viongozi wengine wa Jimbo hilo na
kuahidi kuwa wataendelea kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
0 comments:
Post a Comment