Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Imebainika
kwamba idadi ya wanaume wanaotoa malalamiko yao dhidi ya wenza wao
imeongezeka karibu mara mbili kwa mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka
juzi 2015.
Akitoa
taarifa hiyo ofisini kwake Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na
Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu alisema kwamba
idadi hiyo imeongezeka kutoka walalamikaji 34 mwaka 2015 hadi kufikia 63
mwaka 2016 ambapo ni sawa na 48%.
Alisema ongezeko hilo limetokana na kuenea kwa elimu inayotolewa na askari wa kitengo cha Dawati
kwa watu wa jinsia zote kupitia vyombo vya habari hasa radio zilizopo
jijini hapa. Alisema mbali na radio pia dawati hilo limetoa elimu
kupitia vikao vya wazazi katika shule ya Msingi Osunyai na Shule ya
Msingi Burka zilizopo halmashauri ya jiji la Arusha ambayo imewasaidia
wananchi kujua haki zao na wapi waanzie pindi wanaponyanyaswa ndani ya
ndoa zao.
Mkuu
huyo wa kitengo cha Dawati la Jinsia na watoto mkoa wa Arusha alisema
wengi wa wanaume hao huwa wanafanyiwa ukatili wa Kisaikolojia ambapo
baadhi ya wenza wao wanaonekana kutowathamini lakini wengine kukataa
kushiriki tendo la ndoa.
“Mbali
na Ukatili wa Kisaikolojia pia baadhi yao wanafanyiwa Ukatili wa
kiuchumi ambapo baadhi ya wanawake wenye uwezo kuwazidi waume zao huwa
wakati mwingine wanatoa maamuzi ya kifamilia pengine yakawa na maendeleo
lakini bila kuwashirikisha wenzi wao hali ambayo inawafanya wenzao
wabaini kwamba hali hiyo inatokana na kuzidiwa kipato na hivyo kushindwa
kutengua maamuzi au kutoa ushauri”. Alisema Mkuu huyo wa Dawati.
Mkuu
huyo wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha alitaja wilaya
inayoongoza kwa idadi ya wanaume kuripoti malalamiko yao katika ofisi
yake ni Arusha ambayo ilikuwa na jumla ya walalamikaji 48, Arumeru 8,
huku Ngorongoro ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na walalamikaji watatu.
Wilaya ya Longido ni ya nne ambayo ilikuwa na walalamikaji wawili huku
Karatu na Monduli zilikuwa zina mlalamikaji mmoja kila wilaya.
Mkuu
huyo wa Dawati alitoa wito kwa viongozi wa kata, mitaa, vijiji na hata
vitongoji kuiarifu ofisi yake pindi wanapokuwa na vikao katika maeneo
yao ili waweze kuzidi kusambaza elimu ya ukatili wa kijinsia kwa
wanandoa kupitia vikao hivyo kwani wanaume wengi awali walikuwa hawana
ufahamu kama wao pia wanaweza kutoa malalamiko yao kupitia dawati hilo.
Ofisi
ya Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha mwishoni mwa mwaka jana
imekuwa ikitoa elimu ya ukatili wa jinsia kwa wanafunzi wa shule
mbalimbali za msingi zilizopo katika halmashauri ya jiji la Arusha
ambazo ni Sombetini, Osunyai,Ngarenaro, Kaloleni, Burka na Elerai hali
ambayo imewasaidia wanafunzi hao kupata uelewa mkubwa juu ya ukatili.
Pichani ni Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu
0 comments:
Post a Comment