Home » » WATAALAMU WA CHANJO WANAKUTANA ZANZIBAR KUANDAA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA MARADHI YA POLIO HAYAREJEI TENA NCHINI.

WATAALAMU WA CHANJO WANAKUTANA ZANZIBAR KUANDAA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA MARADHI YA POLIO HAYAREJEI TENA NCHINI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Abdalla akifungua Mkutano wa siku tatu wa matayarisho ya Mpango wa kupambana na maradhi ya Polio Tanzania katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resourt Mbweni.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa matayarisho ya Mpango wa kupambana na Polio wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kutoka Afrika Kusini Dkt. Mercy Kamupira akiwasilisha mada katika mkutano unaozungumzia maradhi ya Polio unaofanyika Zanzibar Beach Resourt Mbweni.
Washiriki wa mkutano unaojadili ugonjwa wa Polio wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Abdalla.Picha na Makame Mshenga-Maelezo.


…………..


Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar 


Wadau wa chanjo wa Tanzania na nchi jirani wapo Zanzibar kwa ajili ya mkutano wa kutathmini maradhi ya polio na matayarisho ya kuandaa mpango wa kukabiliana na maradhi hayo iwapo yatajitokeza.

Akizungumza katika mkutano huo unaofanyika Zanzibar Beach Hotel Mbweni, Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohd Suleiman amesema maradhi ya polio sio tatizao Tanzania kwa sasa, lakini bado hatupo salama kutokana na nchi jirani kuendelea kusumbuliwa na maradhi hayo.

Amesema Tanzania mara ya mwisho kuwa na mgonjwa wa polio ni mwaka 1997 lakini nchi ya Somalia, Jamhuri ya Watu wa Kongo na Nigeria bado wanakabiliwa na maradhi hayo na watu wake wanakuja kwa shughuli mbali mbali za maisha hivyo matayarisho ya kujiandaa ni jambo muhimu.

Amewashauri wazazi kuendelea na utaratibu wa kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya mara baada ya kuzaliwa kupatiwa chanjo zote ili kuhakikisha maradhi hayo na mengine yanayowasumbua hayarejei tena.Meneja wa Kitengo cha chanjo Zanzibar Dkt. Yussuf Haji Makame amesema hali ya chanjo iko vizuri baada ya asilimia 95 ya watoto wanaostahiki kupatiwa chanjo kupatiwa chanjo hizo.

Amesema kitengo hivi sasa kinaendelea kufuatialia kwa karibu watoto wenye umri kuanzia miaka 15 wanapopata ulemavu wa ghafla ili kujua chanzo chake na amewataka wazee wanapobaini kijana wao kupata tatizo hilo kumpeleka hospitali mapema.

Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt. Andemichael Ghirmay ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi kubwa za kupambana na polio na kufanikiwa kupewa cheti maalumu mwaka 2015.Amesema Shirika hilo litaendelea kuunga mkono juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na serikali na ametaka juhudi za pamoja za wadau na jumuiya za kimataifa kuhakikisha polio na maradhi mengine yanayozuilika kwa chanjo sio tatizo tena Zanzibar.

Akifungua mkutano huo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Abdalla amewataka wadau wa chanjo kutoridhika na hatua iliyofikiwa ya kutokomeza Polio bali waendelee kuweka mikakati bora zaidi itakayo hakikisha maradhi hayo hayarejei.

Mkutano huo wa siku tatu unaowashirikisha wataalamu wa chanjo kutoka Shirika la Afya ulimwengu (WHO) na Shirika la kuhudumia watoto (UNICEF) utaundaa Kamati ya Maafa ya polio ya kujiweka tayari wakati wote kukabiliana nayo yatakapo tokea.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa