na Mohammed Mhina,, Zanzibar
WAVUVI wawili raia wa Comoro, wamekutwa katika Kisiwa kidogo cha Pungume nje kidogo ya Zanzibar wakiwa hoi kwa uchovu na njaa baada ya kupotea na kuishi baharini kwa muda wa siku 11 bila ya chakula.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi Zanzibar Kamishna Msaidizi ACP Yusufu Ilembo, aliwataja wavuvi hao kuwa ni Othman Inzudin (24) na Nurdin Ahmed (18) ambao wote ni raia wa visiwa vya Comoro.
Alisema kuwa wavuvi hao walipata msukosuko wakati wakiwa na boti ndogo katika shughuli zao za uvuvi nchini humo ambayo ilipigwa na mawimbi pamoja na upepo mkali na kupotea baharini hatua iliyosababisha kuishiwa mafuta.
Alisema kutokana na hali hiyo, vijana hao walijikuta wakiishi majini kwa muda mrefu bila ya chakula na kunywa maji ya bahari huku wakienda kwa kufuata mwelekeo wa upepo na mawimbi ya bahari hadi walipofika katika kisiwa hicho cha Pungume kilichopo kusini mwa Zanzibar.
Hata hivyo Kamanda Ilembo alisema kuwa baada ya kuokolewa, wavuvi hao walipelekwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kwa matibabu.
Alimtaja kijana Nurdin Ahmed kuwa alipoteza maisha wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.
Alisema Jeshi la Polisi limewasiliana na ubalozi wa Comoro hapa nchini ili kuona uwezekano wa kumsafirisha kijana aliyebaki pamoja na mwili wa marehemu kwenda nchini kwao.
Aidha, Dk. Mohammed Hassan Haji na Dk. Mkasi Khatib Makame, walisema kuwa kifo cha kijana huyo kilisababishwa na uchovu, njaa na hali ya kukata tamaa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment