Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Bila shaka suala linalotawala gumzo na mijadala mingi visiwani Zanzibar hivi sasa ni hatua ya juzi ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kumfukuza kazi Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman Masoud Othman. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini walibashiri kutimuliwa kwake alipopiga kura katika Bunge la Katiba wiki iliyopita na kukataa ibara 22 za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa. Hatua hiyo ilizua mtafaruku mkubwa ndani ya Bunge na kuwafadhaisha wajumbe wa chama tawala ambao tangu awali walitakiwa na chama hicho kupiga kura ya ‘ndiyo’ ili Rasimu ya Katiba iweze kupitishwa.
Mtafaruku ulioibuka bungeni siku hiyo ulisababishwa na mambo matatu makubwa. Kwanza, wakati mwanasheria huyo mkuu wa SMZ akipiga kura hiyo, yalikuwapo mazingira yaliyoonyesha kwamba uwezekano wa kupatikana kwa theluthi mbili za wajumbe kutoka Zanzibar ili kupitisha Rasimu hiyo ya Katiba ulikuwa mdogo sana. Hivyo, uongozi wa Bunge na viongozi wa serikali kutoka pande mbili za Muungano walikuwa katika wakati mgumu wakihaha kwa nguvu zote kupata akidi ya kura.
Pili, mwanasheria mkuu huyo alijitokeza dakika za mwisho kabisa kupiga kura hiyo. Wajumbe, viongozi wa serikali na uongozi wa Bunge waliamini kwamba ingekuwa kura ya turufu na ndiyo ingeamua matokeo na mustakabali wa Rasimu hiyo ya Katiba. Pamoja na msimamo wake wa kutoikubali Rasimu hiyo kujulikana mapema wakati alipojitoa katika Kamati ya Uandishi ya Bunge, bado wajumbe wengi waliamini kwamba katika nafasi yake kama mshauri mkuu wa SMZ katika masuala ya sheria, angelazimika kupiga kura ya ‘ndiyo’ kuiepusha SMZ na aibu ya kuonekana ikikwamisha Rasimu hiyo. Jambo la tatu lililosababisha mtafaruku huo ni sarakasi zilizotawala upigaji kura na zoezi hilo kuonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga nchi nzima, kiasi cha kufanya wajumbe na viongozi wa Zanzibar kuhofia kuonekana wasaliti kwa wenzao wa Tanzania Bara iwapo Rasimu hiyo isingepitishwa.
Hivyo, hata kama hatimaye Rasimu hiyo ilipitishwa, hasira za chama tawala, wajumbe wa chama hicho na viongozi wa Bunge dhidi ya mwanasheria huyo mkuu, zilibaki palepale. Tulishuhudia baadhi ya wajumbe wakionyesha hasira hizo kwa kumzomea na kumtishia maisha mara tu alipopiga kura hiyo, na kulazimika kutoka nje ya Bunge kwa ulinzi mkali na baadaye kurudi Zanzibar mara moja. Ndiyo maana tunasema hatua ya Rais wa Zanzibar kumfuta kazi ilitarajiwa na wengi, hasa tukizingatia kwamba hatua hiyo ya Rais Shein inatokana na mamlaka aliyopewa na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanasema mwanasheria huyo mkuu ametolewa kafara. Hoja yao ya msingi ni kuwa, kama SMZ tangu awali ilisema kupitia Baraza la Wawakilishi kwamba haikuwa na msimamo wowote juu ya Rasimu hiyo ya Katiba, kwa maana kwamba wajumbe kutoka Zanzibar wangekuwa huru bungeni kupiga kura au kufanya uamuzi kadri watakavyoona inafaa, basi mwanasheria huyo mkuu hakufanya kosa lolote kwa kupiga kura ya ‘hapana’.
Vinginevyo, hatua ya Rais Shein kumfukuza kazi inajenga picha kwamba mawaziri na watumishi wa serikali na taasisi zake waliokuwa bungeni, hawakuwa huru kufanya uamuzi kwa utashi wao, bali walipaswa kufuata msimamo na maagizo ya serikali hizo mbili.
Chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment