Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakijafurahishwa na kitendo kilichofanywa na Rais wa Zanzibar. Dk. Ali Mohammed Shein, cha kumfukuza Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud.
Akizungumza na wanachama wa Chadema, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema kitendo cha kuvuliwa uanasheria mkuu Othman, kinadhihirisha kuwa Rais Shein yupo kichama zaidi na siyo kutetea maslahi ya Zanzibar.
Alisema kitendo kilichofanywa na Othman katika Bunge Maalumu la Katiba kwa kukataa baadhi ya vifungu vya katiba inayopendekezwa ni cha ushujaa na ujasiri katika kupigania maslahi ya Wazanzibari na ana imani kuwa uamuzi wake huo ndiyo uliosababisha avuliwe wadhifa aliokuwa nao.
Alisema kilichobaki kwa wananchi ni kuikataa katiba iliyopitishwa na Bunge hilo kama serikali ya Zanzibar ilivyomkataa Othman.
“Chama tawala kilitaka kumtumia mwanasheria huyo kama kikaragosi na kutumikia maslahi ya chama hicho badala ya kuwatumikia wananchi. Lakini kwa kuwa mwanasheria huyo anajielewa, alishindwa kufanya hivyo,” alisema Mwalimu.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema matumaini ya chama chake ni kushirikiana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ili kuhakikisha wanaing’oa CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Ukawa haijavunja vyama vya upinzani, bali upo katika utaratibu mzuri. Na tayari tumeshakubaliana vyama viendelee kujijenga ili viimarishe ushirikiano,” alisema Dk. Slaa.
Viongozi hao walipokelewa na wafuasi wao katika viwanja vya ndege vya Amani Abeid Karume kwa shangwe na nderemo hadi makao makuu ya Chadema, eneo la Darajabovu, ambako askari polisi walifika eneo hilo wakiwa kwenye magari aina ya Land Rover Defender wakibeba silaha na kuwaamuru wafuasi wa chama hicho watawanyike eneo hilo.
Chadema leo inatarajia kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya kwa Mabata Amani, ambako Naibu Katibu Mkuu wake Tanzania Bara, John Mnyika, atahutubia.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment