Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi
akisalimiana na Mwenyekiti wa Vijana wa CCM wa Vyuo Vikuu Zanzibar kwa
ajili ya kulifungua kongamano la CCM kutimia miaka 39 hapo Bwawani
Hoteli Mjini Zanzibar.
Balozi Seif pamoja na Viongozi wengine wa ngazi ya Juu ya CCM na
shirikisho la Vyuo Vikuu Tanzania wakifuatilia mambo yaliyokuwa
yakiendelea kwenye kongamano la kuadhimisha miaka 39 ya CCM ndani ya
ukumbi wa Salama Bwawani.
Baadhi ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi walioshiriki Kongamano ya maadhimisho ya kutimia miaka 39 ya Chama cha Mapinduzi.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano
ya maadhimisho ya kutimia miaka 39 ya Chama cha Mapinduzi. Picha na – OMPR – ZNZ.
NA Othman Khamis Ame, OMPR
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali
Iddi alisema kwamba kazi kubwa iliyopo mbele kwa Vijana wa CCM wa Vyuo
Vikuu ni kutafakari na kulipatia ufumbuzi tatizo la kupungua kwa
ushindi wa Chama hicho ikilinganishwa na chaguzi nyengine zilizopita
nyuma.
Alisema Vijana hao wanapaswa kuelewa kazi kubwa ya chama cha siasa ni
kushinda uchaguzi ili kushika Dola kama inavyoelezwa katika Katiba na
kanuni za Chama cha Mapinduzi.
Akilifungua Kongamano la Vijana wa CCM wa vyuo Vikuu kuadhimisha miaka
39 tangu kuzaliwa kwa CCM hapo katika Ukumbi wa Salama Bwawani Mjini
Zanzibar Balozi Seif alisema Viongozi pamoja na Wanachama wa CCM
wanataka kuona Chama kinaendelea kubakia kuwa kimbilio la Wanawake.
Alisema Chama chochote kitakachojenga tabia ya kudharau kundi la
Wanawake ambalo ndio kubwa katika Jamii hakitokuwa na nafasi ya kushinda
uchaguzi kwa sasa na hata hapo baadaye.
“ Wanawake ni zaidi ya nusu ya Watanzania. Sasa ukilidharau kundi hili
maana yake umejidharau mwenyewe na dhambi hiyo kubwa ambapo isifikie
wakati akatafutwa mchawi wa kulaumiw a”. Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif alilitaja kundi jengine kubwa la Vijana ambalo chama cha
Siasa kinapaswa kuwa na Sera na mfumo bora utakaowavutia Vijana wengi
ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kushinda uchaguzi na huo ndio
mtazamo wa Chama cha Mapinduzi.
Alisema Chama kinategemea kazi hiyo ya kuwavutia Vijana kujiunga kwa
wingi la Chama cha Mapinduzi itasimamiwa na kufanywa na Vijana hao wa
CCM wa Vyuo Vikuu ambao changamoto inayowakabili kwa sasa ni kutoa
mbinu za kutumia ili malengo yaliyokusudiwa yafikiwe mapema
iwezekanavyo.
Aliwashauri Vijana hao wa CCM wa Vyuo Vikuu kujizatiti zaidi katika
ujenzi wa Chama chao kama walivyofanya Vijana Wasomi wa Chama cha zmani
cha ASP wa Young African Social Union (YASU) ambao kazi yao kubwa
ilikuwa kuwakusanya vijana kwa kuwapatia elimu nyakati za jioni.
Balozi Seif alisema kundi la Vijana wa Afro Shirazy Party { Yasu }
lilikuwa na mipango mizuri ya kujenga Chama chao na kupelekea kuanzisha
Magazeti ya Kipanga na Tai pamoja na kujenga Jumba la ghorofa maarufu
Yasu liliopo Mtaa wa Miembeni Mjini Zanzibar.
Akizungumzia uimara wa Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha miaka 39
iliyopita tokea kilipoasisiwa mwaka 1977 Balozi Seif alisema zipo faida
nyingi zilizoimarika kupitia CCM akizitaja kuwa ni pamoja na uimarishaji
wa Muungano, Uongozi wa pamoja kati ya pande mbili za Muungano huo ,
Uchumi pamoja na Demokrasia.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
alifahamisha kwamba historia ya Demokrasia Nchini Tanzania ikiandikwa
haitokamilika bila ya kutoa nafasi ya pekee kwa CCM kutokana na juhudi
zake za kufungua milango ya Demokrasia Nchini.
Balozi Seif alisema Demokrasia madhubuti ndani ya CCM ndio iliyoanzisha
Mjadala wa haja ya kuwa na mfumo wa vyama vingi vya Kisiasa na kupelekea
kufunguliwa milango ya Demokrasia mwaka 1992.
Alieleza kwamba ufunguzi huo wa milango ya Demokrasia Nchini chini ya
Chama cha Mapinduzi umewezesha kuibuka kwa zaidi ya vyama 18 vya siasa
Nchini Tanzania na hatimae kupata usajili wa kudumu kutoka msajili wa
vyama vya Siasa Tanzania.
“ Tofauti ya CCM na vyama vyengine nchini ni uimara wa demokrasia ndani
ya chama chenyewe wakati vile vyengine vinazungumzia demokrasia kwenye
majukwaa tuu ndani ya vyama vyenyewe hakuna kitu kama hicho ”. Alisema
Balozi Seif.
Kuhusu hali ya amani inayoendelea kuwepo Nchini Mjumbe huyo wa Kamati
Kuu ya CCM Taifa alisema kwa vile Amani ni itikadi iliyoota mizizi ndani
ya Chama cha Mapinduzi kila mfuasi wa chama hicho anatakiwa
kuikumbatia kwa mahaba yake yote itikadi hiyo muhimu.
Alisema Chama cha Mapinduzi katika uhai wake wote kimekuwa mstari wa
mbele katika kuhubiri Amani na utulivu na kujiwekea sifa Kimataifa
kikiendelea kuamini kwamba bila ya kuwepo amani Taifa kamwe halitaweza
kuleta Maendeleo.
Kwa vile Amani, Utulivu na Maendeleo ni kama watoto pacha Balozi Seif
alitoa wito kwa Vijana hao wa Chama cha Mapinduzi kutoka Vyuo vikuu
kujaribu wawezavyo kuitumia Taaluma yao katika kuhubiri amani.
Alieleza kwamba Vijana hao wanapaswa kueneza itikadi hiyo katika maeneo
mbali mbali nchini kwa kutumia nguvu zao zote wakibeba ujumbe wa Taasisi
hiyo ya Kisiasa wa CCM ni Amani na Amani ni CCM.
Alisisitiza na kutahadharisha kwamba Jamii imekuwa ikishuhudia kupitia
vyombo mbali mbali vya Habari na Mitandao ya Kijamii jinsi machafuko ya
Kisiasa yanavyozidi kusambaa katika sehemu mbali mbali Ulimwenguni.
Alisema machafuko hayo yanayoleta majanga, maafa pamoja na fadhaa huacha
mayatima na vizuka kadhaa . Hivyo ni vyema yakatumika kama mafunzo kwa
upande wa Wananchi na wafuasi wa vyama vyote Nchini na kuwa tayari
kuepukana nayo kwa gharama zozote zile.
Akitoa Taarifa Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Nchini
Tanzania Nd. Hamid Saleh Muhina alisema lengo la kuundwa kwa shirikisho
hilo ni kuwaandaa Vijana katika mazingira ya kisasa ya sayansi na
Teknoloji ili wajekuwa viongozi bora wa hapo baadaye.
Nd. Hamid alisema mpango huo ndio njia pekee itakayoliwezesha Taifa
kuwa na hazina kubwa ya vijana wasomi watakaokuwa na uwezo kamili wa
kutekeleza majukumu yao katika mfumo wa mtandao wa mawasiliano ya
kisasa.
Akielezea suala la kufutwa kwa uchaguzi Mkuu Mwenyekiti huyo wa
Shirikisho la Vyuo Vikuu Nchini Tanzania alisema Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar { ZEC } ilikuwa sahihi kufanya hivyo baada ya kubaini kasoro
kadhaa zilizofanywa na baadhi ya watu waliosimamia Uchaguzi huo.
Nd. Hamid alivitaka vyama vya siasa ambavyo bado havijaamua kushiriki
uchaguzi wa marejeo kutafakari kwa makini maamuzi yao ili isije fikia
wakati Wananchama wa wakawapotezea haki yao ya Kidemokrasia ya kuchagua
Viongozi wanaowataka.
Mapema Mwenyekiti wa Vijana wa CCM wa Vyuo Vikuu Zanzibar Nd. Khamis
Kheir Ali alisema kwa niaba ya Umoja huo ameipongeza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutekeleza vyema sera zake kiasi kwamba
Jamii ya Watanzania wanaendelea kufaidika na Maendeleo yanayotandikwa.
Nd. Kheir alitolea mfano Sekta ya Elimu ambayo kwa sasa imetoa afueni
kwa Wananchi walio wengi hasa Vijijini kutokana na uamuzi wa makusudi wa
Serikali kufuta ada anazowajibika Mzazi kuchangia sekta hiyo.
Alisema wananchi wameshuhudia uimarishwaji wa miundo mbinu ya sekta ya
elimu unaotoa fursa kwa wananfunzi wa sekondari kupata nafasi za
kuendelea na taaluma zao katika vyuo vya elimu ya juu hapa hapa nchini.
Washiriki hao wa Kongamano la maadhimisho ya kutimia miaka 39 ya Chama
cha Mapinduzi wameuhakikishia Uongozi wa Juu wa Chama hicho kwamba mbali
ya kusimamia uchaguzi wa marejeo ifikapo Tarehe 20 Mwezi wa Machi
lakini pia watashiriki vyema kupiga kura kwenye uchaguzi huo ili
kukamilisha haki yao ya Kidemokrasi.
0 comments:
Post a Comment