WAKATI mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa
kisiasa Zanzibar yakiwa yamekwama, vyama 16 vimeibuka Zanzibar na
kuvitaka vyama vya CCM na CUF kurudi katika meza ya mazungumzo baada ya
kukwama kuundwa kwa serikali ya mseto Zanzibar.
Vyama hivyo vilitoa tamko hilo juzi, katika mkutano wa Baraza la Taifa la Mashauriano la vyama vya siasa lililokutana katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.
Akiwasilisha tamko hilo, katibu mkuu wa baraza hilo, Abdallah Nassor Ally, alisema viongozi wa vyama vya CCM na CUF wanapaswa kurudi katika meza ya mazungumzo ya kutafuta muafaka, ili kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Alisema baraza hilo lipo tayari kusaidia kusukuma mazungumzo hayo, ili kusaidia kupanuka kwa demokrasia pamoja na kukuza hali ya amani na utulivu.
“CCM na CUF virudi tena katika mazungumzo kwa kuangalia maslahi ya taifa na vizazi vyetu, na kufanya hivyo kutavijengea heshima kitaifa na kimataifa,” alisema katibu mkuu huyo.
Vyama vya CCM na CUF vimekwamisha mazungumzo ya kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar baada ya kukwama kwa azimio la kuundwa kwa serikali ya mseto lililokuwa limefikiwa na kamati ya mazungumzo iliyokuwa ikiongozwa na makatibu wakuu wa vyama hivyo Yusuph Makamba wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF.
Alisema wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010, viongozi way CCM na CUF wanapaswa kutafakari kwa busara kubwa juu ya suala la amani ya Zanzibar wakati wa kuelekea katika uchaguzi huo, ili kuhakikisha unafanyika katika mazingira ya uwazi na ukweli.
“Tunataka Zanzibar ipite katika mawimbi ya uchaguzi katika mazingira ya salama na amani kwa maslahi ya wananchi wake,” alisema kiongozi huyo.
Alisema baraza la mashauriano la vyama hivyo kwa muda mrefu lilishindwa kufanya kazi zake kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifedha, ndio maana wakaamua kuomba msaada kwa Rais wa Zanzibar kwa lengo la kuweza kufufua shughuli zake wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi mkuu wa 2010.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdallah Mwinyi, aliwataka viongozi kuzingatia umuhimu wa kulinda amani katika nchi kwa vile wana nafasi kubwa ya kuwashawishi wafuasi wao kutekeleza maslahi ya taifa.
Alisema watu wanaweza kutofautiana kwa itikadi za kisiasa, lakini suala la amani linamgusa kila mwananchi na kuwataka kutumia majadiliano kwa kukosoana bila ya kuathiri umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, mkutano huo ulilazimika kusimama kwa muda baada ya kutokea mvutano mkali kuhusu viwango vya malipo ya fedha kwa viongozi waliohudhuria na sababu ya vyama vya CCM na CUF kutuma maofisa katika mkutano huo badala ya viongozi wa kitaifa.
Naibu Katibu Mkuu wa NLD, Rashid Ahmed Rashid, alitaka kuwekwa wazi kwa hesabu za malipo na kutaka maelezo juu ya upatikanaji wa fedha zilizofanikisha mkutano huo hasa kwa kuzingatia kuwa wameacha shughuli zao za kiuchumi. “Ndugu Mwenyekiti wa kikao, mimi ningependa kupata ufafanuzi kuhusu masilahi yetu yako vipi, mara zote mikutano iliyokuwa ikifanyika Dar es salaam katika mahoteli makubwa tumekuwa tukilipwa posho na nauli, lakini katika barua ya mwaliko imetueleza kuwa hatutolipwa nauli wala tusikodi teksi, sasa tupatie maelezo nani aliyefanikisha mkutano huu?” alihoji Naibu Katibu Mkuu huyo.
Hata hivyo, katibu mkuu wa baraza hilo alisema asilimia 90 ya gharama za mkutano huo zimetokana na juhudi za Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Saleh Ramadhan Feruz na Rais wa Zanzibar Dk Amani Abeid Karume ambaye amesaidia gharama za chakula, ukumbi wa mkutano na nauli kwa wajumbe wa mkutano huo ambao unashirikisha viongozi wote wa kitaifa wa vyama vya siasa vilivyopata usajili wa kudumu
Chanzo;Tanzania
Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment