Home » » JITOKEZENI USAJILI WA ARDHI

JITOKEZENI USAJILI WA ARDHI

WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika usajili wa ardhi ambao utawafanya kuwa na umiliki halali na kuepuka migogoro inayojitokeza sasa.
Hayo yalisemwa na Ofisa Mwandamizi wa Usajili wa Ardhi, Mwanamkaa Abdulrahman wakati alipokabidhi jumla ya kadi mia moja za wananchi waliokamilisha usajili wa ardhi kwa upande wa Mji Mkongwe mjini hapa.
Alisema faida kubwa za kuwa na kadi ya umiliki wa ardhi kwa kiasi kikubwa kunapunguza udanganyifu na kuondosha moja kwa moja migogoro ya ardhi katika jamii na familia kwa ujumla.
“Moja ya faida kubwa ya kuwepo kwa zoezi la usajili wa ardhi ni kuwapa fursa wananchi kuwa na umiliki halali pamoja na kuondosha migogoro ya ardhi pamoja na udanganyifu unaofanywa na matapeli,” alisema.
Alisema lengo la idara ya usajili wa ardhi hadi kufikia mwakani liwe tayari limekamilisha kazi hiyo kwa asilimia 50, lakini kutokana na kasoro mbali mbali ikiwemo elimu ndogo kwa jamii imekuwa kikwazo cha kuchelewesha kuyafikia malengo.
Aidha, alizitaja kasoro nyingine zilizopo ni kuwapo kwa kesi nyingi na malalamiko ya migogoro ya ardhi zinazosubiri kupatiwa ufumbuzi kutoka katika ngazi mbalimbali ikiwemo mahakama.
Alisema migogoro hiyo imechangiwa na kuongezeka kwa thamani ya ardhi inayotokana na kukuwa kwa sekta ya uwekezaji zaidi katika ukanda wa bahari ya fukwe.
“Ndiyo maana Serikali inataka kukamilisha zoezi la usajili wa ardhi ambalo limekwama kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo migogoro ya familia na mengine ya uwekezaji,” alisema.
Suleiman Ali ambaye ni mkazi wa Mji Mkongwe akizungumza katika sherehe za makabidhiano ya hati hizo, alisema amefurahishwa na kukabidhiwa kwa kadi ya usajili wa ardhi ambayo sasa itampa nafasi zaidi kujua umiliki halali wa nyumba yake na kuepuka udanganyifu unaoweza kufanywa na watu.
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa