Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kazi ya kukagua mipaka ya majimbo inayofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(Zec), imepandisha joto la Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Hatua ya uwekaji wa mipaka ya majimbo siyo ya kwanza kufanywa na Tume ya Uchaguzi.
Kipindi cha nyuma, ukaguzi wa mipaka ulifanywa na ikaamuliwa kuunganishwa kwa majimbo ya Malindi na Mkunazini na baadaye kupunguzwa baadhi ya majimbo kisiwani Pemba, kutoka 21 hadi kufikia 18.
Hatua hiyo ilielezwa kuwa ilitokana na ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika 2012 ambayo ilibainisha kuwa hakuna uwiano wa watu wanaoishi katika majimbo 50 ya Unguja na Pemba na kuamuliwa kupitiwa upya kwa mipaka yake.
Tayari Chama cha Wananchi (CUF), kimepinga kazi hiyo na Naibu Katibu Mkuu wake, Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inapaswa kuwa makini katika utekelezaji wa mpango huo na isiwe chanzo cha Zanzibar kuparaganyika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mazrui alisema CUF haoni sababu ya majimbo ya uchaguzi kupunguzwa badala yake yanapaswa kuongezwa kwa kuangalia idadi ya watu katika miji mikubwa na mashamba badala ya mipaka ya majimbo.
Kwa vile Katiba ya Zanzibar bado inatoa nafasi ya kuongeza majimbo ili yafikie 55 badala ya 50 kama ilivyo sasa, alisema kazi hiyo ni vyema ikasitishwa.
Mazrui alisema pamoja na kazi hiyo kufuata masharti ya Katiba ya Zanzibar ya 1984, bado kuna mwonekano wa kisiasa zaidi na kuhoji iweje kambi ya upinzani ndiyo iwe mwathirika zaidi tangu mpango huo ulipoanza kufanyika?
Aliongeza kuwa kazi hiyo isipofanywa kwa weledi, inaweza kuirudisha Zanzibar katika matatizo ya kisiasa.
Msimamo wa CUF
Mazrui alisema CUF haiungi mkono mpango huo endapo utafanywa bila ya kuzingatia ukubwa wa miji na mashamba.
Alisema Zec inapaswa kuzingatia mambo ya msingi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwakani.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na marekebisho katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na kuhakiki watu walioandikisha zaidi ya mara moja.
Alisema kama matatizo hayo yatashindwa kupatiwa ufumbuzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo mkuu mwakani, Zanzibarinaweza kuingia katika matatizo makubwa ya kisiasa na kuiweka nchi katika wakati mgumu ambao utasababisha Serikali ya Umoja waKitaifa (SUK) kutetereka.
Mazrui alieleza kwamba CUF kimemaliza uchaguzi wake wa viongozi na kimeshapanga timu yake ya viongozi watakaopeperusha bendera kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani wakiwa na matumaini makubwa ya kufikia malengo ya kuingia Ikulu ya Zanzibar.
Akizungumzia uchaguzi uliopita, alisema tofauti na uchaguzi mwingine, mwaka 2010 askari polisi na wenzao wa vikosi vya SMZ walifanya kazi vizuri na kuhakikisha kila chama kinapata haki ya kufanya kampeni bila ya vitisho na watu wengi walijitokeza katika uchaguzi huo.
Msingi wa mafanikio
“Mafanikio yalitokana na Serikali kuwa na nia ya kweli ya kufanikisha maridhiano ya vyama viwili vya CUF na CCM, lakini hatua ya Tume ya Uchaguzi kuanza kukata mipaka ya majimbo siyo mwafaka na itateteresha Serikali ya pamoja,” alisema Mazrui.
Alikumbusha kuwa pamoja na Kamati ya Maridhiano kufanya ziara ya mafunzo katika nchi za Ujerumani na Uingereza kuangalia Serikali za umoja wa kitaifa zinavyoundwa na uendeshwaji wake, bado Serikali imeshindwa kufanyia kazi ripoti yake ikiwamo ya muundo wa Serikali ya umoja wa kitaifa kugusa na watendaji wakuu badala ya nafasi za kisiasa pekee.
Alisema uchaguzi wenye kuzingatia viwango vya ubora vya demokrasia, ndiyo mwafaka wa kudumisha amani na Umoja wa Kitaifa na ameishauri Zec kuachana na mpango wa kukata mipaka ya majimbo badala ya kuongeza majimbo ya uchaguzi.
Hata hivyo, alisema Serikali ya Umoja wa Kitaifa pamoja na kufanikiwa kuimarisha hali ya amani, imeshindwa kufikia matumaini ya wananchi ya kushuhudia maisha bora chini ya Serikali ya pamoja.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha alisema kazi ya uwekaji mipaka ya majimbo, ni utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar Kifungu cha 120(1)(3)(5) kinachoipa uwezo kufanya hivyo kila baada ya miaka minane au 10 baada ya kufanyika kwa sensa ya watu na makazi visiwani humo.
Muundo wa majimbo
“Majimbo yote yatakuwa karibu na wakazi kama itakavyoainishwa na Tume, lakini Zec pia inaweza kuepuka shuruti hii kwa kiwango kile kinachofikiriwa kuwa inafaa kwa ajili ya kuzingatia matakwa ya Zanzibar,” inaeleza Sura ya tisa ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.
Mwenyekiti wa ZEC alisema ni haki ya kikatiba kwa chama chochote cha siasa kufungua kesi ya kupinga ukataji wa majimbo, lakini kazi hiyo inafanyika kwa madhumuni ya kukamilisha matakwa ya Katiba ya Zanzibar.
Alisema kazi hiyo itatumia Sh400 milioni na hatua ya kwanza imeshaanza kufanyika ya kukutana na wadau wa uchaguzi, vikiwamo vyama vyenye usajili wa kudumu pamoja na asasi za kiraia visiwa humo.
Tayari Chama cha NCCR- Mageuzi kimetangaza kuwa kina mpango wa kufungua kesi mahakamani kupinga kazi yoyote ya ukataji wa mipaka ya majimbo kwa vile hatua hiyo inaweza kuibua migogoro ya kisiasa ambayo tayari imeshakuwa ni historia.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment