Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ametimiza miaka miaka 15 tangu kufariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999.
Siku hii ni muhimu kwetu hasa wapenda amani na demokrasia. Pia ni siku muhimu kwa wapenda haki, usawa na wale wote tunaoheshimu haki za binadamu, wanaochukia ubaguzi.
Hapa Zanzibar, kuna mengi ya kujifunza kupitia kwa Baba wa Taifa, moja ya jambo ambalo tunapaswa kujifunza ni kuheshimu haki za binadamu, kuchukia ubaguzi na kuwapenda wanajamii wote bila ya ubaguzi, kujali rangi au kabila.
Baba wa Taifa, alichukia ubaguzi, nasi tukiwa wanasiasa, wasomi, wananchi kwa jumla tuweke kando tofauti zetu za kiitikadi kwa kushiriki mchakato wa kura ya maoni na tukichukia ubaguzi kama alivyochukia baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.
Wanasiasa wa Zanzibar wanaowajibu wa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo na siyo kwa porojo, wananchi wamechoshwa na porojo na visa vyao, wanachotaka ni kuona matatizo yao ya kijamii yakitatuliwa kwa mwendo kasi. Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kufanyakazi kwa bidii, kuchukia kila aina ya ovu.
Machi 13, 1995 Mwalimu Nyerere alizungumza na waandishi wa habari wa Dar es Salaam na kukemea vikali tabia ya ubaguzi na akasema: “Makaburu wa Tanzania ni wale wanaojiita wazawa.
“Wazungu wa Afrika Kusini tulikuwa hatuwapingi kwa rangi yao. Tulikuwa tunawapinga kwa ubaguzi wao. Kama una mawazo yaleyale ya kaburu wa Afrika Kusini, wewe ni kaburu tu, ila tofauti yako ni kwamba wewe ni mweusi, lakini ni kaburu tu.”
Sifa kuu Mwalimu Nyerere aliyoipata na kuheshimika katika ulimwengu na leo Tanzania inaitwa ‘Kisiwa cha Amani’ ni jinsi alivyopambana na ukabila yeye na Mzee Karume ambao tunapaswa kuiga kutoka kwao.
Kwa hivyo, yeyote anayeshabikia ubaguzi ni kaburu tu hata kama akiwa mweusi. Hatuna sababu ya kuwaheshimu, kuwalea na kuwaficha, tuwafichuwe ulimwengu uwajue maana ukaburu umekwisha na waliokuwa vinara wa ukaburu, hivi leo wanajutia nafsi zao.
Wakati huu tukiwa katika kumbukumbu ya Baba wa Taifa, tunaweza pia kuvuta picha ya kule tunakotaka kwenda, na hapa nazungumzia suala la ndoto na matuimaini ya kupata Katiba Mpya kama ambavyo mwanaharakati Dk Martin Luther King alivyokuwa na ndoto kule Marekani.
Navuta picha ya mkutano uliohudhuriwa na maelfu ya watu kuhusu haki za kiraia uliofanyika katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Lincoln katika Jiji la Washington D.C Agosti 23 mwaka 1963. DkMartin Luther King katika hotuba yake maarufu ‘I have a dream’ mengi aliyatabiri ambayo yametokea kule Marekani
Hotuba hiyo iliyojaa matumaini kwa watetezi wa haki na demokrasia, kwa wakati ule wengine walitambua umuhimu wa Dk Luther.
Martin Luther King Jr ndoto yake ni ya mchana, lakini Barack Obama amedhihirisha matamshi yale hayakuwa ni ndoto tu.
Nasi katika kumuenzi Baba wa Taifa, tudhihirishe kuwa Zanzibar na Tanzania siyo katika nchi za watu wabaguzi, ni mahali pa kila mmoja kuishi na kuthaminiwa utu wake. Tuwe na ndoto ya kufikia katika kilele cha demokrasia na siyo kuwa na ndoto za kuelendeleza hulka za kikaburu.
Wiki hii pia tumkumbuke kwa kuchukia ubaguzi kama alivyochukia Dk Martin Luther KingJr. Nina hakika aliko Mwalimu anatusikia na anawashangaa wale wanaoendeleza ubaguzi.
Je, wewe utakapoondoka utajivunia nini uko unakokwenda mbele ya haki? Utajivunia matamshi ya kibaguzi, kuwafisadi wenzako, au utajivunia rekodi nzuri ya utu, wema, huruma na upendo kwa binadamu wenzako maana hata wanyama hatutakiwi kuwatendea ukatili.
Zanzibar inakabiliwa na tatizo la umaskini, ukosefu wa ajira na mabadiliko ya tabianchi. Tunategemea kuwasikia wawakilishi wakizungumzia kwa kina masuala yanayowagusa wananchi katika kutafuta njia ya kuyaondoa, siyo wakuongezea mzigo mwengine.
Angalia hali ya umaskini ulivyotamalaki, watu wanaishi chini ya Dola moja ya Marekani kwa siku, jana afadhali kuliko leo.
Huna sababu ya kutafuta vipimo vya kitaalamu kuweza kubaini hali ya umaskini, tembea katika mitaa wanakoishi watu, utaona hali ya maisha ilivyo.
Kuwapo kwa tofauti kubwa kati ya waliokuwa nacho na wale wasiokuwa nacho ni moja ya pengo katika ustawi wa nchi.
Wako wapi wanazuoni wetu waliobobea kwenye uchumi kusaidia raia wenzao.
Lazima sasa watumie usomi wao kukwamua matatizo ya kiuchumi yaliyoikumba nchi yetu.
Tunaona aibu Taifa kama Rwanda kwa kipindi kirefu walikuwa katika vita migogoro, leo uchumi wao unatoa nuru ya matumaini. Angola wamepigana vita miaka mingi, lakini leo wametupita kama tumesimama, tatizo nini wasomi wetu?
Nadhani kuna sehemu yenye tatizo ama kwa wasomi wetu au kwa wanasiasa, maana ukitazama rasilimali za nchi, kwanini tunakuwa katika umaskini kama huu?
Yawezekana pengine wasomi wetu badala ya kuyaelewa matatizo ya jamii na kuyatolea ufumbuzi, wao wanachokijua ni kuyasoma matendo na akili ya wanasiasa kutoa ushauri unaowapendeza.
Kama wanasiasa wetu wangekubali kusikia hata yale wasiotaka kuyasikia kwenye masikio yao, leo tungekuwa tunazungumza lugha nyengine kuhusu umaskini na ukuaji wa uchumi. Wapi wamezoea kusikia yale wanayotaka wao kusikia na kushauriwa sawa kabisa na matakwa yao na siyo kushauriwa sawa na inavyotakiwa?
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment