Home » » BUTIKU: KATIBA INAYOPENDEKEZWA IMEKOSA UJASIRI

BUTIKU: KATIBA INAYOPENDEKEZWA IMEKOSA UJASIRI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku, amesema katiba inayopendekezwa na kukabidhiwa kwa marais wa Jamhuri ya Muungano waTanzania na mwenzake wa Zanzibar imekosa ujasiri kwa vile haijagusa mambo magumu.  

Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE mwishoni mwa wiki, Butiku alisema kuwa wao (tume) walijitahidi kwa kiasi kikubwa kuzingatia maoni ya wananchi na kuyapa nafasi kwenye rasimu ya pili ya katiba, lakini inasikitisha kuona kuwa mwisho wa siku, lengo la kuandika katiba halijatimia kwavile BungeMaalum la Katiba limeondoa mambo mengi na kuandaa katiba inayopendekezwa isiyogusa 'mambo magumu'.

Alisema katiba inayopendekezwa imetupa mambo ya msingi yaliyotolewa na wananchi bila kutoa sababu, kinyume cha vile ilivyofanywa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

"Sisi Tume, mambo ya msingi yaliyosemwa na wananchi tuliyaweka yote... hata yale yaliyokuwa magumu, lakini tukatoa sababu kwa nini tumeyaweka. Na yale ambayo hatukuyaweka tumetoa sababu (pia) ni kwa nini hatukuyaweka. Wenzetu kwenye Bunge naona kama wamezungumza tu wao wenyewe. Hawakuzingatia sana mawazo ya wananchi," alisema.

Akieleza zaidi, Butiku alisema wananchi waliokuwa wanadai katiba mpya waliona kuna kasoro nyingi zikiwamo za kuwapo kwa rushwa, kulaumiana katika uongozi na umaskini; na kwamba katiba mpya ndiyo inayotarajiwa kutoa majibu ya changamoto hizo.

Butiku ambaye alikuwa Katibu wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa miaka 21, alisema vilevile kuwa cha kusikitisha, wananchi hawajapewa nafasi ya kuiandika katiba inayopendekezwa kama walivyokuwa wamedhamiria na kwamba hadi sasa, hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa taarifa zilizotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba zilitumiwa na Bunge Maalum la Katiba.

"Hawakutaka wananchi wazijue. Ndiyo maana walifunga ile tovuti (ya Tume). Zile taarifa tulizokwenda nazo pale bungeni, kwa mfano zile randama, zilikuwa zinafafanua kila kifungu kinasema nini. Wakati tunatoka pale bungeni nyingi zilikuwa zimefichwa," alisema.

UBISHI KUHUSU RASIMU
Butiku alisema inasikitisha kuona kwamba hakuna mwananchi anayepinga kilichoandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake, ubishi kuhusu rasimu ya tume umeibukia bungeni na kuzua kwamba tume haikuzingatia maoni ya wananchi.

Butiku ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, alisema wananchi walikubaliana na Rais kwamba ziko sababu za kutunga katiba mpya ikiwa ni  miaka 50 baada ya uhuru; na wakaamua kwamba katiba hiyo iandikwe na wananchi wenyewe.

Alisema hata sheria iliyotungwa kuwezesha mchakato huo ililenga kuwapa wananchi uhuru na uwazi wa kuandika katiba mpya, na hicho ndicho kilichosimamiwa kikamilifu na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

"Bungeni walichosema, yalizuka maneno kwamba hayo tume inayoyasema siyo mawazo ya wananchi. Ni mawazo ya tume. Kwa hiyo, waseme wameyatoa wapi," alisema.

Alisema kila maoni yaliyokusanywa, tume iliyaandika kwenye ripoti mbalimbali na hata Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria ilipata ufafanuzi wa namna maoni hayo yalivyokusanywa, kuchambuliwa na kuhifadhiwa. Alisema tume yao ilizingatia maoni ya wananchi kwa zaidi ya asilimia 99 kwa kuwa ndivyo sheria iliwataka na ndiyo ulikuwa msingi wa mchakato mzima.

"Kwa hiyo, kinachoshangaza kidogo ni huu ubishi kwamba hayo si maoni ya wananchi. Lakini la pili, ni ubishi kwamba sasa nani ana mamlaka ya kutunga katiba. Safari hii mwenye mamlaka ya kutunga katiba ni wananchi," alisema Butiku.

"Kwa hiyo kazi yetu sisi tume na BMK (Bunge Maalum la Katiba), tulitakiwa kuwa waboreshaji wa maoni ya wananchi... ile rasimu ya kwanza ilivyorudi kwa wananchi katika ngazi ya mabaraza walishiriki kuboresha kile ambacho tume ilikuwa imeandika," alisema, na kuongeza kuwa ushiriki wao (wananchi) umehifadhiwa kwa njia mbalimbali zikiwamo video na maandishi.

"Ndiyo maana pamoja na kelele zote hizi, mimi sijasikia wananchi popote wanasema huo ni uongo... uongo unasemwa bungeni. Sijaona ubishi kwenye TV kusema tume imezua mambo yake, hayo ya kuzua, hayo yamesemwa bungeni," alisema.

Alisema yeye hakutazamia kwamba kutakuwa na ubishi kwani walitazamia watu wangejadili mapendekezo kama yalivyoelezwa kwenye ripoti ya maoni ya wananchi na kufafanuliwa kwenye randama. 

"Maana ipo ripoti ya maoni ya wananchi na ipo ripoti ya maoni ya mabaraza. Kwa hiyo nilitazamia kwamba mtu anasimama pale bungeni akilinganisha na ripoti hiyo," alisema.

Alisema majadiliano ndani ya bunge yalidhihirisha kwamba wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba hawakufanya jitihada za kutaka kujua wananchi walisema nini. 

MAMBO YA WANANCHI
Alisema wananchi walitaka dira ya taifa ijulikane bayana; haki za binadamu na pia walitaka wawe na uwezo wa kuzidai mahakamani.

Alisema wananchi walizungumzia haki nyingi ikiwamo ardhi, pembejeo, bei ya mazao, wafugaji, wasomi, wanawake, watoto, vijana, walemavu na wazee na kwamba ni eneo ambalo wananchi walilizungumza kwa kina.

Alisema wananchi waliujadili kwa kina muundo wa serikali, muungano, bunge, mahakama na madaraka ya rais ambayo walitaka yapunguzwe.

"Eneo kubwa katika mihimili (serikali), lilikuwa madaraka ya rais... kuna maeneo ilitulazimu kuwaeleza urais si mtu, urais ni taasisi. Tukiwaeleza wanaelewa. Lakini hata hivyo, walipenda madaraka ya rais yapungue," alisema.

Alisema kwenye rasimu ya pili, Tume ilimwachia rais madaraka lakini wakimtaka agawane na wengine kwa kuunda tume za ushauri kuhusu uteuzi wa watu wa kada mbalimbali.

Alisema rasimu ilipendekeza ziundwe tume kama ya Mahakama na ile ya Utumishi ambazo zingemshauri katika uteuzi kama wa majaji na kupendekeza baadhi wathibitishwe na Bunge.

Kuhusu wabunge, alisema wananchi walitaka wasiwe na mawaziri na kutaka wawaondoe wabunge wanaoshindwa kutimiza ahadi zao na kutaka mbunge aishi kwenye jimbo lake.Kuhusu tunu, alisema wajumbe wa tume walilazimika kusoma na kutafuta nini maana ya tunu ili kujiridhisha kabla hawajaweka kwenye Katiba.

"Inashangaza kwa sababu tunu wananchi ndiyo walizisema kwa sababu katika katiba ya sasa, hakuna kitu kinachoitwa tunu. Wananchi ndiyo walizisema... walitaka ziwe kwenye katiba ili zisiwepo halafu zikasahaulika."

Alisema wananchi walitaka ukweli uwe tunu kwa sababu uongo umezidi na kwamba walitaka kiongozi akisema uongo wamshtaki, ijapokuwa hawakuweka kwenye tunu.

Alisema wajumbe wa BMK wamekwepa kuziweka kwa sababu zilikuwa zinawagusa baadhi yao. "Ukitazama waliokuwa wanabishana utaweza kuona kwamba mmh, huyu hawezi kuitaka hiyo. Watu wanaofichaficha fedha hawawezi kuzitaka tunu zile," alisema.

ALIYONENA BUTIKU 
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano na Butiku: 

SWALI: Unazungumziaje mapendekezo ya kuzifuta tunu za taifa zilizokuwa kwenye rasimu na kutaka zitungiwe sheria na Bunge kama ilivyopendekezwa kwenye katiba inayopendekezwa?

JIBU: Linashangaza. Silielewi kwa sababu tunu ni wananchi ndiyo waliyozisema. Eeeh… katika katiba ya sasa, hakuna kitu kinaitwa tunu. Eeeh.. lakini wao ndizo wamesema kwamba kitu (hicho), Kiswahili chake ni values, vitu fulani ambavyo ni, eeh… moyoni mwako umevishiba, na hivyo ndivyo dira inayokuongoza wewe na katika mahusiano ya pamoja ndiyo dira huwa tunaweza kusema…kwa hiyo wao, ndiyo wameyataja licha ya kwamba yako mambo mengine ambayo hatujaweka, tumepachika mahali fulani.

Kwa mfano ukweli… ukweli wao walitaka iwe tunu. Sisi tukasema eeeh… kwa sababu walikuwa wanasema uongo umezidi, viongozi wetu waongo,  wanatudanganya. Lakini wengine wakasema kwa sababu Marekani huko ukisema uongo wanakushitaki, eeeh… kwa hiyo ukweli, sisi hatukusema uongo. Ukweli tumeuweka mahali fulani, uwazi eeeh… na zingine hizo walizoondoa kwa kutazama zinashangaza.

Lakini tunu hizi ni za wananchi. Na kusema kwamba unazitungia sheria ni kitu tofauti. Zile ndizo… ni msingi wa uadilifu, ndicho kipimo cha utu, tulikwenda mpaka kwenye dictionary (kamusi) kufungua, kusoma maana ya tunu ni nini ili kweli tuzichague… eeh.

Tuzichague, tuziweke, ni mawazo ya wananchi hayo… eeh. Na, eeh... na kutaka ziwe kwenye katiba ili uweze kuhukumiwa kikatiba. Siyo zisiwemo zikasahaulika, au watu wakakwepa kuziweka kwa sababu wanaona kama zinawahusu.

Ziko zingine (tunu) walizoziondoa unaona mhh…! Ukitazama waliokuwa wanabishana, unaona mhh… huyu hawezi kuitaka hii, wanaoficha ficha fedha hawa na nini hawawezi kuzitaka baadhi ya tunu zile. Kwa hiyo kidogo zaidi zinashangaza, lakini ni vitu vya wananchi kabisa.

SWALI: Tanzania imeendelea kuvuna rasilimali zaidi kulinganisha na enzi za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Hivi sasa kuna migodi mikubwa tisa na mingine ya kawaida 58, lakini bado wananchi wa kawaida hulalamika kuwa ukuaji wa uchumi hauwagusi. Je, una maoni gani kuhusiana na hili?


JIBU: Uchumi una kipimo cha kitaalamu cha kiuchumi.

Wanasema, eeeh… ukikusanya wanaita GDP, eeh… mali yako yote halafu ukaigawa kwa wananchi, then utapata wastani, the average, kuna gross na average. Kwa maana hiyo uchumi unakua.

Lakini maana nyingine ya kupima, si kutumia pato la taifa tu, kwamba unakusanya mapato yake yoote, umeyajumlisha, halafu umeyagawa ukapata wastani, au ukatazama pato lote kwa pamoja ukaona limekuwa, lakini ukigawa kwa wastani unakuta ni kidogo, la kwetu sasa hivi ni kama nadhani… sasa hivi nadhani zimefika laki nane na kitu… something like that, eeh… GDP, eeh.. lakini kikubwa zaidi ni kama pato limekua. 

Wewe kukua huko linaku… limekufikia, umepata kwanza ya jumla… elimu, pato linatosha, elimu ya watoto wako wote ina ubora unaotakiwa, hasa elimu lazima ikufikie wewe na watoto wako, afya, vitu vya msingi kabisa … kwanza elimu, uwezo wa kushughulika na afya yako.


Wewe limekufikia hilo pato, linakuwezesha kufikia wewe na watoto kwa kiwango kinachotakiwa, madawa labda yanatosha, huhangaiki na nini, kwa hiyo zile huduma za umma, zile zinazokuwa za msingi kwa wananchi… maji, kwa hiyo unaona kule kwenye bunge kuna kelele, hilo pato kupitia maji limekufikia, hilo pato kupitia mabarabara hata kama si ya lami limekufikia. 

Kwa hiyo ukienda, eeh… chakula cha kutosha na kilicho bora, umeme, eeh… kuna kitu siku hizi wanaita human development index, mambo ambayo ukiorodhesha, ukiyapitia moja moja, utaona hilo pato la taifa limewawezesha taifa kuliona limekua, lakini vile vile wananchi kuliona limefika katika nyumba zao.


Sasa katika kufika kwenye nyumba zao, halijafika na limeongezeka kidogo wala halijatosha na ukienda kwa bei halisi, ukiacha mfumuko wa bei, ni kama shilingi laki nane, lakini kwa mfumuko wa bei, si laki nane… kwa sababu vitu vingi, havitoshi, kwa hiyo unavinunua kwa mahela meeengi… kwa sababu watu wanavipigania havitoshi.

Kwa hiyo, kwa maana hiyo utasema… tutazame basi inayoitwa umaskini kwa vigezo hivyo, kwamba mimi ni maskini kwa sababu sijapata elimu ya kutosha, mtoto wangu hajapata, hatuna madeski, watoto wetu bado wanakaa chini, bado wanatembea kwa miguu, walimu hawapo wa kutosha, mishahara yao ni midogo, wanagoma, hospitali tunakwenda huko India badala ya kutibiwa hapa.


Mambo yote haya, ukitazama vigezo hivyo, human development index, vigezo ambavyo vinaonyesha, si kukua kwa pato tu, lakini ubora wa maisha ya wananchi umeongezeka kwa kiasi gani, eeeh… kwa hiyo umaskini umepungua kwa kiasi gani… eeeh.

Huko hatujafika, na ndiyo inaleta ubishi kama uchumi umekua.


SWALI: Kuna suala hili la rasilimali gesi ambalo limekuja na changamoto zake. Unafikiri nini kifanyike ili gesi asilia nchini iwe neema na siyo laana kama ilivyokuwa kwa matifa mengine ya Afrika yaliyogundua mafuta na gesi aslia? Nini maoni yako juu ya Watanzania kumiliki rasilimali hii? 

JIBU: Sasa hivi, tulipokuwa hatuna gesi, mpaka juzi juzi hapa, tumeendelea kuhitaji energy, eeeh… nishati. Tumeendelea kuhitaji. Haikutosha, kwa hivyo tulikuwa tunakata miti Mungu aliyotujalia. Ametupa uwezo wa kukoka moto, kuwasha vijiti hivi tunapata nishati, tunapikia.


Kwa hiyo tumekuwa tunakata miti na bado tunakata miti, ukitazama sehemu kubwa ya nchi yetu sasa hivi haina miti, ukienda usukumani, ukienda Sumbawanga huko kulikokuwa na miti mingi, ukienda Mtwara huko kulikokuwa na miti mingi, kote huko, unakuta sehemu nyingine of course ni kukata na kuwauzia wengine wale ambao hawana miti kama Wachina na kupata pesa, kwa hiyo gesi ni nishati.

Gesi itakuwa na maana tu kama itatuondoa kwenye kutumia kuni. Kwamba sasa utapikia gesi, nyumba zetu zote sasa tutapikia gesi, kaya zetu zote zitapikia gesi badala ya kuni. Kwa hiyo miti yetu yote itakuwa salama, oksijeni itaongezeka. Na haya matatizo tunayoanza kuyapata ya mabadiliko ya hali ya hewa yatakwisha.

Na mvua zetu zitastabilise, na hatari ya kukosa maji, kuja kupigania maji itaondoka. Gesi itakuwa na maana kwa maana hiyo, lazima isiwe ni gesi ya kuonyesha kwamba imeingiza fedha kwenye pato la taifa, mfuko umeongezeka wa pato la taifa, dola zimeongezeka kwa pato la taifa, lakini haipenyi ikaenda kutumiwa na wananchi.


Hilo ndilo ule ubishi wa kudhani gesi inaweza kutumika ikaenda kwenye mifuko ya watu ikawafanya ninyi matajiri, ikawa badala ya kilimo, badala ya samaki, badala ya kufuga, badala ya… si kweli.

Ni kama kudhani, dhahabu, mafuta yanaweza kuingia kwenye mifuko ya kila mtu. Na ukitazama Nigeria… Waarabu, mafuta yao yameenda kwenye mifuko ya kila mtu. Pesa hizo zinaweza kutumika kununua tu vifaru, na ndege na nini na kujenga nyumba za wakubwa na kuongeza mishahara, na kadhalika.


Lakini niseme, gesi kama gesi ni lazima iweze kutumiwa na kila family, nyumbani, yaani itakuwa na maana, of course sehemu fulani itauzwa, kusudio ni kuchangia elimu, afya, kuweza kuchangia hospitali, kujenga mabarabara,yale mambo ya pamoja. Lakini tusidhani madini haya ni badala ya matumizi mengine. Siyo kweli.

CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa