Docta Aboubakar kutoka
Blue Health Organisation, akiwaeleza
wanafunzi wa masomo ya Sayansi wa Skuli
za Sekondari walioshiriki semina ya kutoa taaluma juu ya maradhi ya Kensa iliyofanyika
Skuli ya sekondari Haillesselassie, Mjini Zanzibar.
Rais wa Blue Health
Organisation Gora Faki Haji akiwaeleza wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi pamoja
na walimu wao tatizo la maradhi ya Kensa Tanzania katika semina iliyofanyika
Skuli ya Haillesselassie. (Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).
Baadhi ya viongozi wa
Blue Health Organisation wakifuatilia kwa karibu watoa mada katika semina ya
kutoa taaluma ya maradhi ya Kensa iliyofanyika Skuli ya Haillesselassie.
Picha ya pamoja ya viongozi wa
Blue Health Organisation na baadhi ya walimu wa masomo ya Sayansi walioshiriki
semina ya taaluma ya maradhi ya Kensa katika Skuli ys Sekondari
Haillesselassie.(Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar).
Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar .
Wanafunzi wa skuli za sekondari wanaosoma masomo ya Sayansi
na walimu wao Tanzania wamesisitizwa kuongeza juhudi katika masomo yao
na kufanya tafiti zitakazosaidia kugundua matatizo ya afya yanayoikabili
nchi hivi sasa ikiwemo maradhi ya Kensa.
Rais wa Jumuiya ya wataalamu wa fani
mbali mbali za Afya Zanzibar yenye lengo la kutoa taaluma ya maradhi tofauti
kwa wananchi (Blue Health Organisation) Gora Faki Haji ametoa ushauri huo
katika semina ya kuelimisha tatizo la maradhi
ya Kensa iliyowashirikisha baadhi ya wanafunzi wa masomo ya Sayansi wa skuli za sekondari katika
skuli ya Haillesselassie.
Amewaeleza wanafunzi hao kwamba Kensa ni miongoni mwa maradhi hatari
yanayosumbua wananchi wengi Tanzania na idadi kubwa ya watu wanaopata maradhi
hayo hupoteza maisha.
“Takwimu za maradhi ya Kensa kutoka Hospitali ya Ocean Road, inayoshughulikia
maradhi hayo, zinaonyesha kuwa asilimia
14 tu ya watu waliopata Kensa waliweza
kupona,” alisema Gora Faki Haji.
Rais huyo wa Blue Health Organisation omeongeza
kuwa asilimia 66 ya wagonjwa wa kensa waliofika Ocean Road kupatiwa matibabu ni wanawake na asilimia 24
ndio wanaume na hiyo inaonyesha wanawake wanaosumbuliwa zaidi na maradhi hayo.
Amesema pamoja na kuwa hakuna
sababu rasmi inayopelekea kupata kensa moja kwa moja lakini amesema matumizi
ya bidhaa zinazotokana na tumbaku, utumiaji wa pombe na mpangalio usioridhisha
wa chakula unachangia kupata tatizo la maradhi hayo. Amewataka wananchi kujiepusha na
viashiria vinavyoweza kupelekea kupata
kensa na kuwa na utaratibu mzuri wa chakula ikiwemo kutumia zaidi matunda na mboga za majani.
Amewashauri watu kujenga tabia ya kufanya
uchunguzi wa afya zao mara kwa mara na kuwa na
tahadhari wanapopata tatizo la mivimbe
katika miili yao.
Amewahakikishia wananchi kuwa Blue Health Organisation itaendeleza
lengo la kutoa taaluma ya masuala ya
afya kwa makundi tofauti ili waweze
kujua sababu zinazopelekea maradhi na njia za kujiepusha nayo.
Semina hiyo iliwashirikisha wanafunzi
wa skuli za Sekondari Lumumba, Benbella, Hamamni na baadhi ya walimu wa skuli
hizo wanaosomesha masomo ya Sayansi.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment