Na
Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar .
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mhe. Abdilahi Jihadi Hassan amesema Serikali ina mipango
madhubuti ya kuongeza upatikanaji wa samaki ili kukidhi mahitaji ya hoteli za
utalii na walaji kwa ujumla.
Hayo
ameyaeleza katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi
Unguja wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mhe. Ali Salum
Haji.
Amesema
mikakati hiyo ni kuwawezesha wavuvi kuvua katika kina kirefu cha maji ambapo
hivi sasa Wizara yake imeshawapatia mafunzo ya uvuvi wa bahari kuu Vijana 25
katika chuo cha uvuvi Mbegani na hatua ya kupeleka wengine zinaendelea
kulingana na hali ya fedha itakavyoruhusu.
Vilevile
amesema mkakati mwengine ni kuwezesha uzalishaji wa samaki kwa njia ya Ufugaji na
mazao mengine ya Baharini ambapo mikakati hiyo itaongeza upatikanaji wa samaki
kwa wingi na hivyo kupunguza uwezekano wa kuingizwa samaki wasio na uhakika na usalama kwa walaji nchini.
Waziri
Abdilahi amefafanua kwamba itakapotokea uingizaji wa samaki nchini,
watachunguzwa na kuhakikishwa ubora wao na mamlaka zinazohusika ikiwemo Bodi ya
Chakula, Dawa na Vipodozi kabla ya kuruhusiwa kuingizwa nchini.
Wakati
huohuo Waziri Abdilahi ametanabahisha wakati akijibu swali la muakilishi wa
jimbo la Wawi Mhe. Saleh Nassor Juma kuwa uzalishaji wa samaki bado ni mdogo na
unakidhi soko la ndani pekee kwa sasa.
Hivyo
Wizara yake imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuwashawishi Wawekezaji wa
ndani na nje ya nchi kuwekeza katika Sekta ya Uvuvi ili kuongeza uzalishaji wa
samaki ikiwa ni pamoja na kujenga Viwanda vya kusindikia samaki.
Amesema
hayo yatatekelezwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Uwekezaji na Taasisi nyengine
na hivi sasa kuna wawekezaji kadhaa ambao wameonyesha nia ya kuwekeza katika
sekta ya Uvuvi pamoja na kujenga viwanda hivyo.
Mhe.
Abdilahi amesema mazingira ya uwezekezaji yameshawekwa na serikali, hivyo
amewataka wawekezaji kujitokeza ili kutimiza lengo hilo na kusaidia kukuza
uchumi wa nchi kupitia shughuli za uvuvi.
0 comments:
Post a Comment