Na
Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar .
Naibu
Waziri wa Kilimo na Maliasili Zanzibar Mhe. Mtumwa Kheir Mbarak amewataka wananchi
kutokata misitu ya asili na kuchimba mchanga ovyo kwani ndizo sababu zinazopelekea
mabadiliko ya Tabianchi.
Hayo
ameyaeleza katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi
Unguja wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Wawi Mhe. Saleh Nassor
Juma.
Mhe.
Mtumwa amesema ukataji wa misitu ya asili pamoja na uchimbaji mchanga ovyo
husababisha kukosekana kwa mvua za misimu na kuathiri maisha ya wakulima na
wananchi kwa ujumla.
Amesema
ikiwa wananchi wataendelea kukata misitu ya asili hususan mikoko ambayo huzuia
upepo wa Bahari na kupandisha kina cha maji, kutapelekea Visiwa vya Zanzibar
kukatika vipandevipande na maji kujaa hadi katika makaazi ya watu kama ilivyo
hivi sasa kwa baadhi ya vijiji hapa zanzibar.
“Na
athari za ziada zitafuata baadae ikiwa wataendelea kukata hasa mikoko ambayo
inazuia upepo wa Bahari na kupandisha kina cha maji, matokeo yake visiwa
vitakatika vipande vipande na maji yatapanda mpaka viamboni (katika makaazi ya
watu) na mfano hai hayo sasa yanatokea katika vijiji vya Jozani, Mziwanda, Koowe
na kwengine kwingi”, alieleza Naibu Waziri Mtumwa.
Aidha
ametanabahisha kuwa Serikali imechukua juhudi mbalimbali katika kuhakikisha kwamba
athari za mabadiliko hayo zinapungua, miongoni mwa juhudi hizo ni kuanzishwa
vikundi mbalimbali vya jamii husika kwa matakwa yao wenyewe kutunza misitu ya
asili iliopo katika maeneo yao wanayoishi Unguja na Pemba, Udhibiti wa msumeno
wa moto kutotumika mpaka kwa ruhusa na kibali maalumu.
Sambamba
na hayo Mhe. Mtumwa amesema kuwa Serikali imeanzisha miradi mbalimbali ili
kuondokana na tatizo hilo ikiwemo mradi wa TASAF unaojishughulisha na mpango wa
kujenga miundombinu ya umwagiliaji maji ambao umesaidia umwagiliaji kwa kilimo
cha Mpunga, Mboga na Matunda, pia wakulima kusomeshwa njia bora za ukulima na
kuwapa fedha za kuanzishia mashamba kupitia mradi wa PADEP, ASSP na ASDPL.
Akiongezea
Mhe. Mtumwa amesema serikali imeanzisha sheria maalumu za kuzuia ukataji wa
miti ovyo ikiwemo sheria ya COFMA ambayo imetungwa ili kudhibiti wanaoharibu
misitu kiholela.
Mhe.
Mtumwa amewataka viongozi na wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi za Serikali
katika kupiga vita ukataji wa misitu ya asili na uchimbaji mchanga ovyo ili
kuondokana na janga la Tabianchi na ukosefu wa mvua za misimu na kutilia mkazo
kilimo cha kisasa pamoja na upandaji wa miti.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.