Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar,
ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein leo amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya Urais wa
Zanzibar na kueleza matumaini yake ya kuendelea kuchaguliwa kutokana kuwa na
sifa zote za kuwa Rais wa Zanzibar.
Dk. Shein alichukua
fomu hiyo katika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar iliopo Kisiwandui mjini Unguja
majira ya asubuhi akikabidhiwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali
Vuai akiwa ni mwana CCM pekee kuchukua fomu katika ngazi hiyo tokea kuanza mchakato.
Viongozi mbali
mbali walimshindikiza Dk. Shein akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Idd pamoja na mkewe Mama
Mwanamwema Shein na viongozi wengine mbali mbali ambapo mara baada ya kuchukua
fomu alipata fursa ya kuzungumza na wanaCCM na wananchi waliofika katika hafla
hiyo.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alitoa shukurani kwa wanaCCM waliojitokeza kwa wingi katika
hafla hiyo kwa lengo la kuimarisha chama hicho huku akieleza sababu kubwa
zilizomfanya kuchukua fomu hiyo ikiwa ni pamoja na kuendeleza hatua za
maendeleo yaliofikiwa pamoja na kuendeleza wimbi la ushindi wa chama hicho kama
ilivyo kawaida katika kila uchaguzi mkuu.
Dk. Shein alisema
kuwa anaamini ataendelea kuungwa mkono na wananchi walio wengi pamoja na kuwa
na sifa, uwezo, uzoefu wa kutosha katika chama na utendaji wa kazi katika Serikali
zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wa CCM Zanzibar kwa uwamuzi wao wa
kimaendeleo wa kuendeleza harakati za Mapinduzi kwani yote hayo ni kwa ajili ya
maendeleo ya Zanzibar huku akitoa shukurani kwa wanaCCM na wananchi kwa
kuendelea kumuunga mkono kwa kumchagua mwaka 2010 sambamba na kuendelea kuwa na
matumaini ya kumchagua tena mwaka huu.
Dk. Shein alisema
kuwa katika kipindi chote alichoingia madarakani mafanikio makubwa yameweza
kupatikana ikiwa ni pamoja na kutekeleza Ilani ya CCM, ambayo hadi hii leo
tayari imeshatekelezwa kwa asilimia 90 na kuwa na matumaini ya kufikia asilimia
100 baada ya miezi minne yapo.
Aidha, Dk. Shein
alishangazwa na baadhi ya viongozi kujipa sifa na kujisifu ndani ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kuwa yote yanayofanywa ndani ya Serikali hiyo huamuliwa
na Baraza la Mapinduzi ambalo huwahusisha viongozi wote Serikali.
Alisema kuwa
iwapo CCM itampitisha kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya chama hicho aliahidi kuendelea
kufanya kazi katika wazifa huo kwa ufanisi mkubwa bila ya woga, hofu huku akisisitiza
jambo la msingi ni kuyalinda na kuyaendeleza Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari
12, 1964 sambamba na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Dk. Shein pia
alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi na wanaCCM pamoja na wapenda amani wote
kuwa atawashughulikia kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi wale wote
watakaotaka kuvuruga amani na utulivu uliopo.
Alisisitiza kuwa
hatochelea kumchukulia hatua yeyote atakaevuruga amani huku akieleza azma ya kuendelea kusimamia uchumi ambao umeendelea
kukua kwa kiasi kikubwa katika uongozi wake.
Aidha, alieleza
kuwa ataendelea kuutetea Muungano wa Serikali mbili na kuahidi kuudumisha kwani
ndio Sera za CCM . Pia alieleza azma yake ya kuendelea kusimamia Utawala Bora,
kuendeleza mchakato wa uchimbaji gesi na mafuta hapa Zanzibar sambamba na
kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji.
Alisema kuwa
wakati anaingia madarakani uchumi ulikuwa umekwua kwa asilimia 5.2 lakini
katika uongozi wake hadi hivi leo uchumi umeendelea kukua kwa asilimia 7.2
hukua akieleza kuwa kwa mwezi kulikuwa kunakusanywa Tsh.Bilioni 13.5 wakati hivi sasa kwa mwezi
kunakushanywa Tsh. Bilioni 39 sambamba na kukua kwa pato la mtu mmoja mmoja.
Dk. Shein alisema
kuwa ataendelea kuisimamia misingi ya uchumi imara ili izidi kuimarika ikiwa ni
pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume mnamo
mwezi wa Oktoba mwaka huu sambamba na uwekaji wa taa katika uwanja wa ndege wa
Pemba kazi ambayo inaendelea pamoja na azma ya kuujenga majengo ya kisasa
katika uwanja huo.
Pia, Dk. Shein alieleza kuwa azma ya kujengwa Bandari mpya
ya Mpigaduri ipo na hivi sasa imefikia hatua nzuri kwani azma hiyo ilianza
katika Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dk. Salmin Amour Juma katika mpango wa
kuwa na Bandari Huru na sio kama inavyozungumzwa na watu wengine.
Alisema kuwa hivi
sasa tayari mradi huo umeshakubaliwa na michoro, ramani na fedha tayari
zimeshatafutwa
Katika mazungumzo
kati yake na waandishi wa Habari Dk. Shein aliwaeleza mipango ya Zanzibar ya
kuwa na miji minne ya kisasa, kuendelezwa kwa Maeneo Huru ya Vitegauchumi,
kuongeza kasi ya utendaji kazi, kuendeleza michezo pamoja na miundombinu yake,
kuliimrisha Shirika la Meli, Bandari, ununuzi wa meli nyengine ya mafuta na
mambo mengineyo.
Nao viongozi wa
CCM wakitoa shukurani na pongezi zao kwa Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar
walieleza kuwa Rais Bora anatoka CCM na sio katika chama chengine chochote cha
upinzani na Dk. Shein ndio wanaemtarajia kuwa Rais wa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment