Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAFANYABIASHARA wote nchini wametakiwa kutopandisha
bei za bidhaa zao katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani bila ya sababu za msingi na
kuwafikiria wananchi hasa wanyonge kwani hatua hiyo ni kinyume na malengo ya
Serikali ya kupunguza unafuu wa kodi kwa bidhaa za chakula.
Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar
katika risala yake ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani aliyoitoa kwa wananchi kupitia
vyombo vya habari.
Katika risala
yake hiyo Alhaj Dk. Shein alisema kuwa wafanyabiashara wasivutiwe na kutaka
kupata faida kubwa, bali wawafikirie wananchi wenzao kwani si jambo la busara
kuutumia mwezi huu kwa kuwapandishia bei wananchi, hasa wanyonge.
Alhaj Dk. Shein
alisema kuwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani shughuli za biashara huimarika
zaidi hivyo aliwasihi wafanyabiashara kuendelea kuzingatia sheria na kusisitiza
biashara zote zifanywe katika maeneo yalioruhusiwa ili kuepusha usumbufu na
msongamano usio wa lazima.
Aliwataka
wafanyabiashara pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Manispaa kwa mji wa Unguja
na Mabaraza ya Mji wa Pemba, kuongeza juhudi zao katika kuimarisha usafi wa
miji kwani uzoefu unaonesha kuwa katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani taka
huongezeka.
Alieleza kuwa
Serikali imeendelea kushirikiana na wafanyabiashara katika utekelezaji wa Sera
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutoa unafuu wa kodi katika uingizaji
nchini bidhaa muhimu za chakula ikiwemo mchele, unga wa ngano, sukari na tende.
Alhaj Dk. Shein
alieleza kuwa lengo la uamuzi huu wa Serikali ni kuhakikisha kuwa chakula cha
kutosha kinakuwepo katika kipindi chote cha Mwezi wa Ramadhani na kinapatikana
kwa bei nafuu zaidi.
Akieleza kuhusu
wakulima wenye tamaa ambao huamua kuleta sokoni mazao ambayo hayajapea, Alhaj Dk.
Shein alizitaka taasisi zinazohusika kusimamia taratibu na utekelezaji wa
Sheria ya kumlinda mtumiaji, ikiwa ni pamoja na kuwaepusha wananchi kuuziwa
bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umemalizika.
“Tuna wajibu wa
kujiandaa na kuweka azma ya kuzidisha Ibada kwa wingi ikiwa ni pamoja na
kufanya mambo yote ya Kheri, kusali sala za faradhi na sunna na kujifunza
pamoja na kusoma sana Kurani”,alisema Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk.
Shein aliendelea kuiagiza Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA) na Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kufanya kila jitihada ili iwapatie maji
wananchi kwa kutumia magari katika maeneo yote ambayo huduma hiyo ina upungufu.
Pamoja na hayo, Alhaj
Dk. Shein alieleza kuwa katika mazingatio ya kufanya wema na kufuata maadili
yanayotukuzwa katika mwezi wa Ramadhani, wananchi wanapaswa kuzingatia umuhimu
wa kudumisha na kukuza amani na utulivu.
Alisisitiza kuwa
Ibada ya saumu inahitaji kuwepo kwa utulivu wa nafsi ili kuwapa watu
kuitekeleza Ibada hiyo yenye malipo makubwa kwa MwenyeziMungu ambapo katika
suala hilo watu wote wana wajibu wa kusimamia amani na utulivu ili utekelezaji
wa ibada hiyo usiathirike.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza kuwa katika kufunga yapo mambo ya kuharibu funga ya mfungaji ambapo
miongoni mwa mambo hayo ni kusema uongo na kufitini watu, hivyo aliwataka
wananchi kujiepusha na mambo ya aina hiyo na badala yake wazidishe mapenzi
baina yao, wahurumiane na kusaidiana katika ambo ya kheri.
Wakati huo huo,
Alhaj Dk. Shein aliwasihi wenye kumiliki mikahawa washirikiane na waumini
wanaotukuza Mwezi huo katika kuondoa kero ambazo zinaweza kuwasababishia karaha
wanapoitekeleza Ibada ya funga.
Aliwataka
wananchi kuheshimu utamaduni walionao wa kuheshimu dini, jambo ambalo
limechangia kudumu kwa amani ya nchi tangu kale na dahari na kusisitiza kuwa
kila mmoja anapaswa kuhakikisha kuwa Mwezi wa Ramadhani unaheshimiwa kwa
vitendo.
Pia, aliwataka
wazazi kuwa waangalifu kwa watoto wao nyakati za usiku, ili wawe na nyendo
njema pamoja na kuwashajiisha kufanya ibada na kudumisha darsa misikitini. Aidha,
alivitaka vyombyo vya ulinzi kuimarisha doria za ulizni katika maeneo mbali
mbali, hasa kwa wakati ambao watu wengine wanakuwa katika shughuli za Ibada.
Alhaj Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuwakumbusha madereva kuzingatia sheria za usalama wa
barabarani kwa kutoendesha gari na vyombo vyengine kwa mwendo wa kasi kwa
kisingizio cha kutaka kuwahi kufutari sambamba na kupakia abiria zaidi jambo
ambalo huhatarisha usalama wao.
Sambamba na hayo,
Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwatakia wananchi kheri, rehema na baraka
za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kumuomba MwenyeziMungu kuwapa wananchi uwezo
wa kuendeleza Ibada za saumu na ibada nyengine katika mwezi huu pamoja na
kudumisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano.
Alhaj Dk. Shein,
Alimuomba MwenyeziMungu kuwapa baraka wale wote wanaojiandaa na watakaojaaliwa
kwenda kuhiji mwaka huu kuwajaalia kheri na safari ya salama.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment