Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambi rambi Kadhi
Mkuu wa Tanzania Bara Samahat Sheikh Abdulla Yussuf Mnyasi, kufuatia
kifo cha Sheikh Issa Shaaban Simba, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania
Bara.
Katika salamu
hizo za rambi rambi, Dk. Shein alisema kuwa amepokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa ya kifo
cha Sheikh Issa Shaaban Simba, Sheikh
Mkuu na Mufti wa Tanzania Bara kilichotokea tarehe 15 Juni mwaka huu.
Salamu hizo za
rambirambi pia, zilieleza kuwa kifo cha Sheikh Issa Shaaban Simba ni msiba
mkubwa kwa Waislamu na Watanzania wote kwa jumla.
Akimuelezea
Sheikh Issa Shaaban Simba katika salamu hizo, Dk. Shein alieleza kuwa Marehemu
Sheikh Simba alikuwa ni kiongozi muadilifu mwenye taaluma kubwa na mwenye
kupendelea umoja, mshikamano na elimu. ‘Sote tutazikosa busara na hekima zake
kufuatia kifo hicho”,zilieleza salamu hizo.
Kwa niaba yake
Dk. Shein na wananchi wote wa Zanzibar, anatoa salamu za rambirambi kwa ndugu,
Waislamu wote na wananchi wa Tanzania
nzima kwa jumla.
Aidha, salamu
hizo za rambirambi zilimuomba Kadhi Mkuu wa Tanzania Bara, Samahat Sheikh
Abdalla Yussuf Mnyasi kuzifikisha kwa ndugu, jamaa na marafiki wote wa Marehemu
Sheikh Simba.
“Tunawahakikishia
kwamba sote tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha msiba’,zilieleza
salamu hizo.
Pamoja na hayo, salamu
hizo zilimuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu Sheikh Issa Shaaban
Simba mahali pema peponi. Amin.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment