Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya
Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha
sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwaleta Madaktari kila baada ya
miaka miwili hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar katika mazungumzo kati yake na Madaktari kutoka Jamhuri ya Watu wa China waliomaliza muda wao wa kazi hapa nchini
waliofika Ikulu kwa ajili ya kumuaga Rais wakiongozwa na Balozi Mdogo wa nchi
hiyo anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Mhe. Xie Yunliang.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alieleza kuwa utamaduni wa kuwaleta Madaktari bingwa kutoka
China ni wa kihistoria ambao umeanza tokea mwaka 1965 baada ya nchi hiyo kuleta
wataalamu wake mbali mbali hapa Zanzibar
wakiwemo Madaktari bigwa hatua ambayo inaendelea hadi hii leo.
Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na wananchi wake wanathamini na
wanazipenda huduma mbali mbali zinazotolewa na Madaktari hao hapa Zanzibar.
Dk. Shein pia, alitumia
fursa hiyo kueleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya China na Zanzibar na
kuahidi kuendelezwa na kudumishwa, huku akisisitiza kuwa nchi hiyo imeweza
kutoa mchango mkubwa katika mafanikio ya sekta ya afya hapa nchi.
Aidha, Dk. Shein
alieleza mafanikio yaliofikiwa katika kutoa huduma za afya hapa Zanzibar ambapo
hivi sasa huduma nyingi ambazo zilikuwa zinapatikana nje ya Zanzibar hivi sasa
zimekuwa zikipatikana kwa kutolewa kwa ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na huduma
za upasuaji wa maradhi mbali mbali yakiwemo ubongo na uti wa mgongo.
Dk. Shein alieleza
kuwa mbali ya huduma hiyo ya afya waliyoitoa kwa wananchi wa Zanzibar pia,
aliwapongeza Madaktari hao kwa kulifanyia kazi wazo lake la kipaumbele katika
kinga juu ya maradhi mbali mbali kazi ambayo waliifanya kwa ufanisi mkubwa.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alitoa pongezi zake kwa Serikali ya China chini ya kiongozi wake Rais
Xie Jingping kwa kuendelea kuisaidia na kuiunga mkono Zanzibar katika
kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo hivi sasa inatekelezwa
ukiwemo ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani Pemba, Ujenzi wa Uwanja wa
Mao tse Tung na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid
Amani Karume Zanzibar.
Nao Madaktari hao
kwa upande wake walitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini
ya uongozi wake Dk. Sheim wananchi pamoja na uongozi na wafanyakazi wote wa
Wizara wa Afya kutokana na ushirikiano mkubwa waliopata wakati wote.
Kiongozi wa
Madaktari hao, Dk. Liu Yaping akitoa
shukurani kwa niaba ya Madaktari hao alisema kuwa timu hiyo ya Madaktari 25
kutoka China ambayo imefanya kazi kwa muda wa miaka miwili hapa nchini kwa
bidii na mashirikiano makubwa kati yao na madaktari Wazalendo kwa lengo la
kutoa huduma kwa wananchi wa Zanzibar.
Alisema kuwa mbali
ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Zanzibar, Madaktari hao kwa msaada mkubwa wa Serikali ya Jamhuri ya
Watu wa China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wameweza kuanzishwa kitengo
cha Uchunguzi wa Mfumo wa njia ya chakula katika hospitali ya MnaziMmmoja hapa
Unguja na kitengo cha viungo na ajali huko katika Hospitali ya Abdalla Mzee
Pemba.
Pamoja na hayo,
Madaktari hao walieleza kuwa katika juhudi zao za kutoa huduma za afya hapa
Zanzibar waliweza kufanya ziara mbali mbali kwa ajili ya kutoa huduma vijijini,
kutoa elimu ya afya katika vyombo vya habari kupitia Shirika la Utangazaji la
Zanzibar ZBC, kutoa vitabu kwa ajili ya Chuo cha Afya Mbweni pamoja na kufundisha
wanafunzi katika chuo maalum cha Afya Zanzibar.
Pia, walieleza
kufanikisha wazo la Dk. Shein alilowapa hapo
Agosti 19 mwaka 2013 walipokuja kujitambulisha wazo la kutoa kipaumbele katika
suala zima la kinga ya afya.
Aidha, Madaktari
hao walieleza kuwa tokea nchi hiyo kuanza kuleta Madaktari wake hapa Zanzibar tayari imeshatimia
miaka 50 na kusisitiza kuwa umri huo si tu wa kutoa huduma za afya bali pia, ni
umri ambao umeimarisha urafiki na udugu baina ya pande mbili hizo..
Pamoja na hayo,
Madaktari hao walieleza jinsi walivyofurahishwa na maisha yao wakati wote
walipoishi Zanzibar kwa kutembelea sehemu mbali mbali zikiwemo za kitalii na
kujihisi wako nyumbani kwa muda wote na kutoa pongezi kwa ukaribu wa Wazanzibar
na kueleza kupendezewa na maisha ya amani na utulivu wanayoishi Wazanzibari.
Nae Balozi Mdogo
wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Mhe Xie Yunliang alimueleza Dk. Shein
kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ambapo pia,alitumia fursa hiyo
kumueleza maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Abdalla Mzee huko Mkoni Pemba
kuwa unaendelea vizuri.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
0 comments:
Post a Comment