Home » » BULEMBO KUPIGA KAMBI ZANZIBAR UCHAGUZI WA MARUDIO

BULEMBO KUPIGA KAMBI ZANZIBAR UCHAGUZI WA MARUDIO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais John Magufuli.
Wakati mazungumzo ya kutafuta muafaka wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana yakiendelea kufanyika , Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya mwenyekiti wake, Abdallah Bulembo, imejipanga kupiga kambi visiwani Zanzibar kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.
 
Chama hicho kimeridhia kurudiwa kwa uchaguzi huo, huku chama kikuu cha upinzani visiwani humo CUF ambacho mgombea wake ni Seif Shariff Hamad kikikataa kurudiwa kwa uchaguzi huo na kutaka atangazwe mshindi kwa kuzingatia uchaguzi mkuu uliopita ambao matokeo yake yalifutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa madai ya kufanyika udanganyifu.
 
 Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana mara baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza kuu la jumuiya hiyo, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo taifa, Abdallah Bulembo, alisema baraza hilo limeridhia jumuiya hiyo kuhamia Zanzibar kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi mkuu wa marudio.
 
“Tutahamia Zanzibar tutakapotangaziwa ni tarehe ngapi imepangwa uchaguzi huo kufanyika,” alisema Bulembo.
 
Aidha, alisema kikao hicho cha baraza kuu pia kilimpongeza Rais John Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.
 
WALIOHAMIA UPINZANI
Kuhusu  kujaza nafasi za watu waliohamia vyama vya upinzani, Bulembo alisema baraza limeteua watu kujaza nafasi za walioondoka CCM kwenda vyama vya hivyo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana wakiwa wajumbe wa baraza hilo.
 
“Mkoa wa Kagera mjumbe wa baraza kuu alihamia Chadema, mkoa wa Pwani alihamia CUF, mkoa wa Njombe alihamia ACT-Wazalendo, kwahiyo nafasi zile tumepitisha majina matatu matatu ili yarudi kwenye mikoa kujaza hizo nafasi,” alisema.
 
Bulembo pia alisema amemteua, Shehe Hamis Hamdani, kuwa mjumbe wa baraza hilo kutoka Pemba na katika nafasi ya mjumbe wa kamati ya utekelezaji taifa baraza limemchagua Jaffari Mwenyemba ambaye ni Meya wa Manispaa ya Dodoma na Godfrey Mheluka kuwa Naibu Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Bara.
 
WIKI YA WAZAZI
 Bulembo alisema mwaka huu wiki ya wazazi itafanyika mkoani Morogoro  na kwamba sherehe za miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM zitakazofanyika mkoani Singida, jumuiya hiyo itapiga kambi huko kufanya kazi za chama.
 
Kuhusu elimu, Bulembo alisema Baraza limeagiza watu wote wanaohusika na ubadhirifu katika shule zinazomilikiwa na jumuiya hiyo wapelekwe mahakamani.
 
Alisema kuna shule zimefanyiwa ukaguzi na kubainika kuwapo na ubadhirifu wa fedha nyingi na watumishi wote waliohusika watapelekwa mahakamani.
 
CHANZO: NIPASHE.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa