Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Dk. John Magufuli
Mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, Mohamed Raza,
amesema ufisadi umefikia hatua ya kutisha Tanzania kutokana na viongozi
kushindwa kusimamia miiko na maadili ya uongozi.
Raza alitoa tamko hilo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari huko Malindi, Zanzibar, kuhusu hatua za kupambana na ufisadi
zinazoendelea kuchukuliwa na Rais Dk. John Magufuli, tangu
alipochaguliwa Oktoba, mwaka jana.
Alisema kwa muda mrefu viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia
serikali wameshindwa kupambana na rushwa na ufisadi kutokana na
kuporomoka kwa miiko na maadili ya uongozi na kupeana vyeo kwa
kuangalia urafiki na ushemeji.
“Rais wetu amerejesha matumaini makubwa kwa wananchi na heshima ya
serikali baada ya muda mrefu watu kupeana vyeo kwa kuangalia urafiki na
ushemeji kwa sababu ya kuporomoka maadili ya uongozi,” alisema.
Kwa mujibu wa Raza, wakati umefika serikali kuzifanyia uchunguzi
kesi za zamani za ufisadi zikiwemo za ununuzi wa Rada, EPA na ESCROW na
wahusika wafikishwe katika mikondo ya sheria.
Alisema kashifa hizo za ufisadi hazikufanyiwa uchunguzi wa kina
kutokana na mazingira ya serikali kwa wakati huo, lakini serikali ya
awamu ya tano imeonyesha kwa vitendo uchungu wake dhidi ya ufisadi.
Alisema wabunge wana nafasi nzuri ya kumsadia Rais katika kikao
kinachoanza mwezi huu kutokana na hotuba yake kugusa kero mbalimbali
vikiwemo ya ufisadi, urasimu na uwajibikaji kwa watumishi wa serikali.
"Wito wangu wabunge wa vyama vyote wajadili hotuba ya Rais wetu
kwani ina mambo mengi ya kuleta heshima kwa Tanzania. Muhimu wazungumze
kwa uwazi na ukweli," alisisitiza.
Pia alisema inasikitisha kuona watu walikuwa wanakwepa kulipa kodi
ya mabilioni ya fedha wakati kuna Watanzania wanashindwa kupata huduma
muhimu za kijamii na wengine kula mlo mmoja kwa siku.
Aliwaonya baadhi ya watu kuwa kama wanadhani kasi ya Rais Dk.
Magufuli ni nguvu ya soda, wanajidanganya kutokana na msingi wa
uwajibikaji unaoendelea kuenea katika ngazi mbalimbali za uongozi wake.
Hata hivyo, alisema kuwa kasi ya uwajibikaji inapaswa kuungwa mkono
pia na serikali ya Mapinduzi ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kuondoa
urasimu katika upatikanaji wa huduma za jamii na vitendo vya uzembe kwa
watumishi wa umma.
Kuhusu kero za Muungano, alisema anaamini iwapo Wazanzibari
watajenga hoja, Rais Magufuli ana uwezo mkubwa wa kuondosha kero za
Muungano kwa wakati muafaka.
Akizungumzia mkwamo wa uchaguzi Zanzibar, alisema mazungumzo
yanayoendelea yana umuhimu mkubwa kuthaminiwa na kuungwa mkono na
wananchi katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.
Alisema viongozi wanaoshiriki mazungumzo hayo ni wazito hivyo
utafika wakati watapata ufumbuzi hivyo ni muhimu wananchi kuwa na moyo
wa subira.
CHANZO:
NIPASHE.
0 comments:
Post a Comment