Home » » Ofisi za ZEC zapigwa komeo

Ofisi za ZEC zapigwa komeo

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Mwenyekiti ya wa ZEC, Jecha Salim Jecha.
By Hassan Ali, Mwananchi

Zanzibar. Wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikiwataka wananchi kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio visiwani humo, hakuna shughuli zinazoendelea kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambayo inatakiwa itangaze mchakato huo.

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alisema wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani utarudiwa katika tarehe itakayotangazwa na ZEC, ambayo ilifuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka jana kwa madai sheria na kanuni zilikiukwa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye ofisi hizo zilizoko Maisara mjini Unguja, umebaini kuwa kumekuwa hakuna shughuli zinazoendelea na hata Hoteli ya Bwawani, ambako ZEC ilikuwa ikitangazia matokeo hakukuwapo na taarifa zozote kama chombo hicho kilikuwa kikifanya shughuli zake.

“Sisi hatuna mamlaka ya kueleza chochote. Watendaji wote hawapo inakuwa shida,” alisema mfanyakazi mmoja wa ZEC ambaye alikuwa nje ya ofisi hiyo huku mlango ukiwa umefungwa.

Alisema wahusika wote wa sekretariati na watendaji, wakiwamo makamishna wa tume hiyo, hawafiki ofisini tangu mwenyekiti Jecha Salim Jecha alipotangaza kufuta uchaguzi Oktoba 28, 2015.

takriban miezi mitatu iliyopita.

Jecha mwenyewe amekuwa haonekani hadharani tangu atangaze uamuzi huo. Mara pekee aliyojitokeza ilikuwa siku ya Mapinduzi. gazeti hili liliwahi kwenda nyumbani kwake na kijijini kwake, lakini halikufanikiwa kumpata.

Msemaji wa ZEC, Maalim Idrisa Haji Jecha alipatikana baadaye jana, lakini akasema kwa sasa yuko likizo na hawezi kuhusika au kuongelea mambo ya kiofisi.

“Mie niko likizo sasa sina la kusema, watendaji au wasemaji wa Tume ni angalau sekretari (katibu) ambaye ndiye mkurugenzi, ila hao wengine sidhani wala hawana mamlaka ya kueleza chochote,” alisema.

Kuhusu taarifa na azma ya kurudiwa kwa uchaguzi, Maalim Idrissa alisema: “Rafiki yangu, siwezi kukuambia chochote. Mimi hizo habari nimezipata hivyohivyo kupitia magazetini, sielewi ukweli wake.”

Hali hiyo ya ZEC kutoendelea na shughuli zake inawashangaza wananchi.

“Haya mambo hayaeleweki wala hayakubaliki kwa hapa tulipofikia maana huu ni mchezo unachezwa wa kupinda demokrasia huku ulimwengu ukishuhudia. Hili haliwezi kuitumbukiza nchi katika matatizo?” alihoji Omar Haji Vuai wa Chaumma aliyekuwa kwenye ofisi kuu ya Zanzibar jana.

Omar alisisitiza kauli ya Chaumma kuwa haikubaliani na hatua yoyote ya kurudia Uchaguzi wa Zanzibar.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa