Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT),
ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Asha Bakari
Makame, amefariki dunia.
Asha (65) alifariki dunia jana alfajiri huko Dubai, Falme za Kiarabu
alipokwenda kwa mapumziko kwa mtoto wake akitokea India kwa matibabu ya
ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua.
Akithibitisha kifo cha mwanasiasa huyo ambaye pia aliwahi kuwa Waziri
wa Wanawake na Watoto Zanzibar, kaka wa marehemu Mbarouk Bakari Makame,
alisema Asha alikutwa na mauti hayo akiwa katika maandalizi ya kurejea
nchini.
Alisema baada ya kupokea taarifa ya kifo hicho, hivi sasa familia ipo
katika maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu kuletwa nchini
ambapo unatarajiwa kuwasili leo saa 10 jioni kwa ndege ya Shirika la
Qatar Air Ways.
Makame alisema baada ya kuwasili mwili wa marehemu utapelekwa
nyumbani kwake eneo la Jang’ombe na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho
saa 4 asubuhi katika makaburi ya Kianga nje kidogo ya mji wa Unguja.
Asha aliyewahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (Viti Maalumu) na
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, atakumbukwa kwa kuwa na misimamo
isiyoyumba ndani ya chama chake cha CCM pamoja na kuibua maneno ya
mipasho kwa wajumbe wa Kambi ya Upinzani ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Kwa nyakati tofauti mipasho yake imeibua hisia kali ndani na nje ya
baraza hilo na kusababisha kambi ya chama tawala na ile ya upinzani
kutupiana vijembe.
HISTORIA YA ASHA
Mwanasiasa huyo machachari visiwani Zanzibar atakumbukwa kwa uwezo
wake wa kupambana na vyama vya upinzani, hasa Chama cha Wananchi (CUF),
kupitia majukwa ya siasa na hata ndani ya Baraza la Wawakilishi.
Mwanzoni mwa mwaka 2000 akiwa ndani ya Baraza la Wawakilishi, aliibua
msemo maarufu kwamba ‘Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haiwezi kutolewa
kwa vikaratasi’.
Msemo huu aliurudia tena mapema mwaka juzi wakati wa vikao vya Bunge
Maalumu la Katiba mjini Dodoma lililokuwa likijadili utungwaji wa Katiba
Mpya.
Ndani ya Bunge hilo, Asha aliibua hoja nzito ikiwamo kuibuka na msemo
wa ‘kuufyatua’ wakati akijibu mapigo ya aliyekuwa mjumbe mwenzake,
Ismail Jussa Ladhu.
JUSSA AMLILIA
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu,
alisema chama chao kimepokea taarifa hizo kwa masikitiko na kusisitiza
Asha alikuwa ni mwanasiasa mwenye uwezo wa kujenga hoja ndani ya Baraza
la Wawakilishi katika kile anachokiamini.
“Alikuwa ni mhimili mkubwa ndani ya chama chao CCM, alikuwa mjengaji
mzuri wa hoja ambazo zingeweza kuleta manufaa kwa chama chake,” alisema
Jussa.
Alisema CUF kitashiriki kikamilifu katika mazishi ya mwanasiasa huyo,
kwani chama hicho hakina tabia ya kuchanganya siasa na mambo ya kiutu.
CHANZO: MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment